
RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa amesema kuwa viongozi wa kizazi kipya wameacha kufuata misingi ya waasisi wa taifa na badala yake wanafuata yao, jambo alilodai kuchangia kuleta nyufa katika amani iliyodumu kwa takribani miaka 51 ya uhuru.
Alisema kuwa wakati wa utawala wake wa miaka kumi, alijitahidi kufuata misingi iliyoachwa na Baba wa Taifa, hayati Julius Nyerere tofauti na sasa ambapo viongozi wa kizazi kipya wanafuata misingi yao.
Mkapa alitoa kauli hiyo jana mjini Bukoba wakati akitoa salamu zake katika ibada ya misa takatifu ya kumsimika Askofu wa Jimbo la Bukoba, Desiderius Rwoma, ambaye amehamishwa kutoka Jimbo Katoliki la Singida kuchukua nafasi ya Askofu Nestory Timanywa aliyestaafu.
“Uongozi wa sasa wa kizazi kipya hauwezi kutufikisha popote katika kulinda amani iliyopo, hivyo yafaa viongozi wajao katika kuiongozi nchi hii kufuata misingi ya Mwalimu Nyerere aliyoiacha katika kulinda amani ya nchi,” alisisitiza.
Alisema kuwa ni muhimu kwa viongozi kufuata misingi iliyoachwa na viongozi waliopita jambo ambalo litasaidia kupunguza hali ya uvunjifu wa amani inayoanza kujitokeza sasa katika jamii ya Watanzania.
Mkapa alisisitiza juu ya kuwepo hali ya kuheshimiana miongoni mwa wanadamu, akisema kwamba ikiwa kila mtu atatambua kuwa aliumbwa na mwenyezi Mungu, hana budi kuhakikisha anamheshimu mwenzie bila kujali itikadi wala dini yake.
“Sisi wote ni wamoja, tumeumbwa kwa mfano wake Mungu na yatubidi kupendana bila kujali itikadi za kidini ambazo zinaweza kuleta machafuko na uvunjifu wa amani ambayo inatuweka kwa pamoja sisi Watanzania,” alisema Mkapa.
Katika hatua nyingine, Mkapa amewataka wananchi kuhakikisha wanakuwa watulivu katika kipindi hiki cha mchakato wa kuandika katiba mpya ili iwe na mwongozo mzuri kwa kila Mtanzania na kuondoa minong’ono ambayo imejengeka kwenye jamii kwa sasa.
Naye Askofu Rwoma pamoja na kuwashukuru waamini wa jimbo la Bukoba, alisema kuwa kwa hivi sasa Tanzania inahitaji maombi na busara za kiuongozi ili kuongeza amani na utulivu ambayo jamii imeizoea.
Askofu huyo aliongeza kuwa kinacholeta maendeleo katika jamii ni ushirikiano, mshikamano, upendo na kuheshimiana ambavyo kwa pamoja vinaleta amani na kwamba vikikosekana maendeleo hayawezi kuwepo kwa wanadamu.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na maaskofu zaidi ya 30 kutoka majimbo mbalimbali akiwemo pia Balozi wa Baba Mtakatifu nchini, viongozi wa serikali na vyama na maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Kagera na mikoa jirani.
Uteuzi wa Askofu Roma ulifanywa Januari 15 na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI. Huyu anakuwa askofu wa nne wa jimbo hili tangu kuanzishwa kwake mwaka 1960.
Wengine waliowahi kuwa maaskofu wa jimbo hili ni hayati Mwadhama Laurean Kardinali Rugamwa, Gerevazi Nkaranga na Nestory Timanywa ambaye ameshika wadhifa huo kwa miaka 39.
Sumaye afyatuka
Naye Danson Kaijage anaripoti kutoka mjini Dodoma kuwa Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye amesema nchi haiwezi kutawalika kama rasilimali zake zitaendelea kumilikiwa na watu wachache huku watu wengi wakiendelea kuwa masikini.
Sumaye alitoa rai hiyo jana wakati wa uzinduzi wa santuri ya sauti ya kwaya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Kitivo cha Elimu (COED).
Alisema kuwa machafuko ambayo yanajitokeza kwa sasa yanatokana na kundi kubwa la Watanzania kuwa masikini, hali iliyosababishwa na kundi dogo la watu kuwa matajiri huku kundi kubwa likibaki masikini.
“Ukumbuke binadamu yeyote aliyekata tamaa na mwenye njaa hatawaliki hata umwambie nini,” alisema Sumaye.
Aliongeza kuwa nchi kwa sasa imeingia katika migogoro mingi kutokana na huduma za jamii kuwa duni ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa chuki za matabaka kati ya watu wenye uwezo na wale wasiokuwa nao.
“Kumbuka kilichotokea kule Mtwara, watu walichoma nyumba za watu moto hata wale ambao walikuwa wabunge siku nyingi kisa tu ni mwendesha pikipiki ambaye aligongwa, japo hakufa lakini hilo lilitokana na hasira kwa kufikiri kuwa wanatendewa hivyo kutokana na umasikini wao,” alisema.
Jambo jingine ambao Sumaye alilielezea kama chanzo cha migogoro nchini ni kuwepo kwa matabaka ya huduma za kijamii kwa madai kuwa kuna kundi dogo linapata huduma nzuri huku kundi kubwa la Watanzania wanapata huduma mbovu.
Alisema ili kujenga usawa ni lazima Watanzania wapatiwe huduma zinazofanana za kielimu, kiafya na nyinginezo.
SOURCE: TANZANIA DAIMA
Comments
Post a Comment