
Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, kuwasilisha jana nakala za mitaala bungeni
kama alivyoahidi wiki iliyopita, hofu ya kujiuzulu Mbunge wa Kuteuliwa,
James Mbatia imegubika NCCR-Mageuzi.
Waziri Kawambwa aliwasilisha mitaala ya
elimu ya awali, msingi na sekondari ya mwaka 2005 bungeni, kabla ya
kuanza kipindi cha maswali na majibu kama alivyoahidi Januari 31.
Muda mfupi baada ya hilo kufanyika
bungeni Dodoma na Bunge kuamua kuihakiki kama haijachakachuliwa, hofu
ilitanda NCCR-Mageuzi, kutokana na kiapo cha Mbatia kwamba
ikiwasilishwa, atajiuzulu ubunge.
Kutokana na hofu hiyo, Katibu wa
Uhusiano na Uenezi Taifa, Kitengo cha Vijana wa NCCR-Mageuzi, Deogratius
Kisandu, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akielezea kutokubaliana
na hatua ya Mbatia kujiuzulu.
Kuwasilishwa kwa mitaala hiyo,
kulitokana na hoja binafsi ya Mbatia ambaye ni Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi akidai kwamba Serikali haina mitaala na ndiyo maana elimu
nchini inaendeshwa kwa udhaifu.
Mbatia aliitaka Serikali iwasilishe
mitaala hiyo Januari 31 na kuahidi kuwa kama ingewasilishwa, angekuwa
tayari kujiuzulu. Kutokana na madai hayo yaliyoendana na kiapo, Naibu
Spika, Job Ndugai, alimwagiza Dk Kawambwa kuileta mitaala hiyo bungeni
jana.
Hata hivyo, kabla ya kuwasilishwa kwa
mitaala hiyo, Mbatia alifanya mkutano na waandishi wa habari bungeni na
kusema kwa kuwa Serikali ilishindwa kuwasilisha mitaala Januari 31,
iliyoletwa jana, itakuwa imechakachuliwa.
Kamati ya Bunge Kutokana na kauli hizo
za Mbatia, baada ya Dk Kawambwa kuwasilisha mitaala hiyo kama
alivyoahidi, Ndugai aliunda Kamati ya watu sita kuichunguza kama ni
halisi au imechakachuliwa.
Naibu Spika alisema maadam mitaala hiyo
iliwasilishwa mezani kwake, jukumu la kujua uhalisia si kazi ya Mbunge,
bali ya Bunge na kwa mantiki hiyo, akaunda Kamati kuangalia uhalisia
wake.
Alitaja wajumbe sita wa Kamati hiyo kuwa
ni Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii za Bunge, ambaye ni Mbunge
wa Viti Maalumu, Margaret Sitta (CCM) na Mbunge wa Kibiti, Abdul
Marombwa (CCM).
Wengine ni Mbunge wa Chwaka, Yahya
Kassim Yahya (CCM); Mbunge wa Viti Maalumu, Bernadetha Mshashu (CCM);
Mbunge wa Karatu, Israel Natse (Chadema) na Mbunge wa Gando, Khalif
Suleiman Khalifa (CUF).
Pamoja na kuunda Kamati, Naibu Spika
alimruhusu Mbatia kushirikiana na Kamati hiyo pamoja na watendaji kutoka
serikalini, ili kuhakiki mitaala kama imechakachuliwa au la.
Alisema kama Kamati hiyo itabaini
mitaala ni halisi, wataigawa kwa wabunge kwa ajili ya matumizi yao. Hofu
NCCR Pamoja na kuwa Mbatia hajazungumzia kujiuzulu kwake, wala Bunge
halijamtaka achukue hatua kutekeleza kiapo hicho, Kisandu katika taarifa
yake alisema:
“Sisi vijana wa NCCR-Mageuzi tunasema
hatutakubali Mwenyekiti wetu ajiuzulu ubunge, eti kwa sababu mitaala
imepatikana, kwani Serikali ilikuwa wapi kuitoa tangu miaka yote hiyo
mpaka Mbatia ‘akakomalia’ ndipo ipatikane? “Hajiuzulu mtu hapo, kwa nini
hawakupeleka siku ile aliyotaka Mbatia? Je, kama wamekwenda
kuitengeneza, kuna uhalali gani wa Mbatia kujiuzulu?
Tuamke Watanzania,” alieleza Kisandu.
Alisisitiza kuwa kama Serikali ingepeleka mitaala siku ambayo Mbatia
aliiomba, wangekubaliana naye ajiuzulu, lakini kwa kuwa muda umepita,
hawakubali ajiuzulu.
“Hakuna haja ya kujiuzulu. Waulize
walimu na wakufunzi wao na maprofesa wao kama wamewahi kuiona pamoja na
kuwa na kozi inayohusu mitaala vyuoni, hebu nenda shuleni na vyuoni kama
utaiona.
“Sasa Mbatia kafungua ukurasa mpya,
shinikizo lake limewezesha hata wadau waone mitaala ya elimu ya
Tanzania. Rai yangu magazeti yaichapishe ili nasi tufaidi yaliyomo,”
alishauri.
SOURCE:-HABARI LEO
Comments
Post a Comment