
Amefungwa kwa kosa la kutishia kumuua
kwa maneno Mwinjilisti wa usharika huo, Christopher Daniel (36).
Mwinjilishi Daniel alimfungulia Loinyeye mashitaka Julai 12 mwaka jana
katika Mahakama ya Mwanzo ya Emaoi iliyoko wilayani Arumeru katika Mkoa
wa Arusha.Juni 30 mwaka jana, mzee huyo wa kanisa alikamatwa wakati
akiwa katika kikao cha hesabu za harambee.
Akisoma hukumu Ijumaa iliyopita katika
mahakama hiyo, Hakimu Denis Shayo, alisema mahakama imebaini kuwa
mshitakiwa alikuwa na chuki kubwa na mlalamikaji (Daniel) kwa madai ya
kutumia vibaya fedha za harambee zaidi ya sh milioni 20, zilizochangwa
Machi 11 mwaka jana na Mbunge wa Moshi, Philemon Ndesamburo.
“Chuki hiyo imetokana na ubadhirifu wa
fedha za harambee zaidi ya shilingi milioni 24 ambazo zilipatikana
wakati wa harambee ya ujenzi wa kanisa la usharika huo,” alisema Hakimu
Alisema mahakama imesikiliza ushahidi wa
pande zote na imeridhika na ushahidi wa mazingira na kuona kuwa
kulikuwa na chuki kati ya mshitakiwa na mlalamikaji, hivyo imemtia
hatiani mshitakiwa kuwa alitenda kosa hilo.
Hakimu Shayo alisema pamoja na shahidi
wa pili wa mlalamikaji, Elphans Mereji (46) kukana kutofahamu njama za
kupanga kumuua mwinjilisti Daniel, lakini alikana hivyo baada ya kubaini
kuwa njama hizo zilijulikana.
Alisema shahidi wa kwanza wa upande wa
mlalamikaji Christopher Ngungati (54) aliieleza mahakama kwamba Mereji
alikwenda nyumbani kwake na kumweleza kwamba kipo kikundi cha watu,
wakiongozwa na Loinyeye kimeandaa majambazi kwa lengo la kutaka kumuua
Mwinjilisti Daniel na ameahidiwa kupewa Sh 300,000 kwa kazi hiyo.
Hakimu Shayo alisema mashahidi wa upande
wa mshitakiwa, Emilina Stephen (36), Loning’o Loshinongi (45) na Dora
Seuri (3), wote waliieleza mahakama kuwa kesi iliyofunguliwa mahakamani
hapo ilikuwa ya chuki.
Kwa mujibu wa Hakimu, mashahidi hao
walisema kwamba mshitakiwa alifunguliwa kesi hiyo na mwinjilisti kwa
lengo la kupunguza makali ya mzee huyo wa baraza, kuacha kumfuata na
kutakiwa kutoa hesabu za harambee ya sh milioni 24.
Hakimu alisema pamoja na kusema hivyo
mahakamani hapo, mashahidi hao walishindwa kutoa ushahidi wao kama
mwinjilisti huyo anadaiwa fedha hizo. Kutokana na hali hiyo,mahakama
iliridhika na kuona kwamba kulikuwa na ushahidi wa mazingira na kuamua
kumtia hatiani mshitakiwa kwa kifungo cha nje cha miezi sita na ndani ya
kifungo hicho mtuhumiwa ametakiwa kutotenda kosa lolote.
Hata hivyo, Loinyeye amepinga hukumu
hiyo na kusema sababu zilizotolewa na hakimu kwamba mashahidi wake
hawakutoa vielelezo vya ushahidi wa ubadhirifu dhidi ya mwinjilisti
haina msingi.
Loinyeye alisema kesi iliyofunguliwa
mahakamani hapo ni ya kutishia kuua kwa maneno dhidi yake na siyo
ubadhirifu wa fedha za harambee na mashahidi walitoa ushahidi ni kwani
nini kesi hiyo ilifunguliwa katika mahakama hiyo na wengine kukana
kupanga njama hizo.
‘’Ninakata rufaa katika Mahakama ya Wilaya kupinga hukumu hiyo kwani haki yangu imechakachuliwa,’’alisema Loinyeye .
Mgogoro wa KKKT Usharika wa Ngaramtoni,
Jimbo la Arusha Magharibi huo uliotokana na ubadhirifu wa fedha, uliwahi
kuripotiwa na gazeti hili, ambapo Mkuu wa Jimbo, Mchungaji Godwini
Lekashu alituhumiwa kutumia vibaya fedha hizo za harambee. Hata hivyo,
Lekashu aliripotiwa kukana shutuma hizo na kusema yeye siyo mmoja wa
watuhumiwa.
Mkuu wa KKKT, Askofu Dkt Alex Malasusa
aliunda Kamati ya maaskofu sita kutoka nje ya Dayosisi ya Kaskazini Kati
Arusha, kuchunguza chanzo cha migogoro ili kupata undani wa tatizo na
hatimaye kufikia hatua ya kuumaliza.
Hata hivyo migogoro ndani ya Dayosisi
hiyo iliibuka mara baada ya Mchungaji Kiongozi, Philemon Mollel wa
Usharika wa Ngateu, Jimbo la Arusha Magharibi kufukuzwa kazi na
kusimamishwa kufanya shughuli za kichungaji katika kanisa hilo, kwa
madai yasiyovumilika ndani ya kanisa.
SOURCE; HABARI LEO
Comments
Post a Comment