MITAALA YA ELIMU YAMNG'OA MKURUGENZI

MOTO uliowashwa na Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR Mageuzi), kuhusu utata wa mitaala ya elimu nchini, hatimaye umemng’oa Mkurugenzi wa Elimu Tanzania, Dk. Paul Mushi.


Katika kikao kilichopita, Mbatia aliwasilisha hoja binafsi kuhusu udhaifu wa mitaala ya elimu na kulitaka Bunge liunde kamati teule ya kuchunguza udhaifu uliopo katika elimu.

Habari za kuaminika ambazo MTANZANIA imethibitishiwa mjini Dar es Salaam jana, zinasema baada ya tuhuma hizo, Dk. Mushi mwenyewe, aliandika barua ya kujiuzulu kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.

Habari hizo, zinasema nafasi ya Dk. Mushi, tayari imekaimiwa na Dk. Leonard Akwilapo, ambaye awali alikuwa Mkurugenzi wa Elimu, Matirio na Maendeleo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Dk. Mushi alisema: “Ni kweli nimejiuzulu, kwa hiari yangu, ninaomba suala hilo lisihusishwe na sakata la mitaala ya elimu kwa sababu ipo na hilo halina ubishi.

“Hakuna shinikizo lolote, nimejiuzulu kama alivyofanya Papa Benedict XVI (Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani)… niliandika barua ya kujiuzulu kwa waziri na tayari nimepata majibu yangu, tangu Februari 13, mwaka huu.

Naye Dk. Akwilapo kwa upande wake, alikiri kukaimu nafasi hiyo, lakini hakutaka kuingia kwa undani zaidi, akiomba atafutwe baadaye, kwa kile alichodai alikuwa barabarani akiendesha gari.

Dk. Akwilapo alitangazwa kukaimu nafasi hiyo, katika kikao cha wafanyakazi kilichofanyika katikati ya wiki hii, ambapo Dk. Mushi aliitumia nafasi hiyo kuagana na wafanyakazi wenzake.

Naye Mbatia, alipoulizwa kuhusu kujiuzulu kwa kigogo huyo, alisema kwa kifupi tu: “Siku zote uhuru utatuweka huru na hiyo imethibitisha wazi vielelezo vyangu vilikuwa sahihi na kamwe tunapaswa kutanguliza utaifa kwanza katika majukumu yetu ya kila siku.” 

Juhudi za MTANZANIA kumpata Waziri Dk. Kawambwa, hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa. Hoja binafsi ya Mbatia
Kwa kutumia kanuni ya 57 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la 2007, Mbatia alisema elimu inayotolewa katika taifa hivi sasa, ina udhaifu mkubwa na imesababisha uduni wa elimu katika ngazi mbalimbali.

Aliliambia Bunge kuwa kitengo kilichopo chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kinachotoa ithibati kwa vitabu vya kiada na ziada - Educational Materials Approval Committee (EMAC), kimeshindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo.

Alisema kitengo hicho, kimesababisha ‘mafuriko’ ya vitabu vinavyopotosha dhana ya elimu kwa taifa.    

Alitolea mfano vitabu vingi vya kiada vilivyopewa ithibati na EMAC, kwamba vina makosa mengi ya kitaaluma na hata mfumo wa uandaaji na usambazaji wa vitabu hivyo una harufu ya rushwa. Uhalali wa Mitaala
Itakumbukwa baada ya hoja hiyo, Spika wa Bunge, Anna Makinda, aliunda kamati ndogo ya Bunge kuchunguza uhalali wa mitaala iliyoletwa na Waziri Dk. Kawambwa.

Ingawa kamati hiyo ilisema, mitaala iliyoletwa na waziri ilikuwa sahihi, Mbatia alipinga, akisema imechakachuliwa ili kulinda uovu wa watendaji.

Alisema mitaala hiyo iliyoletwa, haikuwa na ISB namba, ambayo ni lazima kwa vitabu vyote vinavyoandikwa Tanzania, ikiwemo mitaala.

Mbatia pia alihoji vitabu vya mitaala kukosa saini ya Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ambaye wakati huo, alikuwa ni Dk. Mushi mwenyewe.

Hoja nyingine ya Mbatia, ilikuwa ni mtaala wa sekondari kuonyeshwa ni wa Tanzania bara, wakati suala la elimu ya sekondari ni la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, Mbatia alidai kuwa mitaala aliyoomba tangu Oktoba 30, mwaka jana ni ya mwaka 1997 hadi 2005, lakini ule ulioletwa na Serikali ni wa mwaka 1998 hadi 2008.

source:mtanzania

Comments