MBUNGE WA MTWARA MJINI AKALIA KUTI KAVU CCM

 
WAKATI ghasia za kupinga gesi iliyovumbuliwa Mtwara zimetulia, Mbunge wa Mtwara Mjini, Hasnain Murji (CCM), amekalia kuti kavu na huenda akang’olewa uanachama na hivyo kupoteza ubunge, Tanzania Daima Jumatano limebaini.

Habari ambazo gazeti hili imezipata, zilisema kuwa mbunge huyo amekuwa akitajwa kuwa chanzo cha vurugu hizo zilizosababisha vifo vya watu wanne, akiwemo askari polisi mmoja na hasara ya zaidi ya sh bilioni tatu kutokana na nyumba, magari na mali zingine zilizoteketezwa kwa moto.
Habari kutoka ndani ya CCM, zilisema kuwa tayari Murji alishaitwa na uongozi wa juu ya chama hicho tawala kujadili namna anavyohusishwa na machafuko hayo.
“Suala la Murji limeshafika ndani ya vikao vya chama, kwa bahati mbaya hadi sasa hatuna Kamati Kuu (CC) na Kamati ya Maadili ambayo inapaswa kumjadili na kutoa mapendekezo yake,” alisema mtoa habari wetu.
Kwa mujibu wa ratiba ya CCM iliyopatikana mjini hapa, Halmashauri Kuu (NEC), inatarajia kuanza kikao chake mjini hapa Februari 9, ambapo Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kutangaza Kamati Kuu (CC) mpya, aliyoahidi kwamba itakuwa na sura mpya.
Kwa mujibu wa habari hizo, kutokuwa na Kamati Kuu, kumesimamisha maamuzi mengi yakiwemo yaliyofikiwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula katika kupitia malalamiko ya wagombea wanaodaiwa kushinda kwa rushwa kwenye uchaguzi wa ndani ya chama.
Hata hivyo, Murji mwenyewe amesema kuwa wananchi wake ndio watakaoamua hatua yoyote itakayoamriwa na chama.
Mbali ya Murji, wengine waliokalia kuti kavu ni mawaziri wawili; George Mkuchika wa Ofisi ya Rais - Utawala Bora na Hawa Ghasia wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Mawaziri hao waandamizi ambao ni wazawa wa Kusini na wabunge katika maeneo yao, wamekuwa katika shutuma kutoka kwa wananchi wenzao, wakidaiwa kutojali maslahi ya watu wa hali ya chini, huku wakituhumiwa kutoa kauli tata zilizochochea vurugu hizo.
Mawaziri hao ni kama wanakalia 'kuti kavu' si kwa nafasi zao za uwaziri tu, bali hata ubunge kama wataonesha nia ya kutaka kuwania tena mwaka 2015.
Dalili mbaya za wazi juu ya nafasi za mawaziri hao kwa wananchi wa maeneo yao, zilianza mwaka jana wakati wa ziara ya Katibu Mkuu CCM, Abdulrahaman Kinana, ambako Ghasia alinukuliwa akidiriki kutamka kwamba gesi haitowasaidia wana-Mtwara.
Ghasia na Mkuchika walitarajiwa kuwa katika ziara ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda mkoani Mtwara, mahsusi kutuliza hali tata katika eneo hilo kutokana na nafasi zao, lakini hawakushirikishwa, jambo ambalo linazidi 'kupigilia msumari' katika 'jeneza' la wanasiasa hao katika harakati zao za kisiasa na maswahiba zao kuelekea 2015.
Pinda alikutana na wadau mbalimbali mkoani humo na aliwashirikisha mawaziri wengine bila ya Ghasia na Mkuchika, hatua ambayo inaelezwa kuwafurahisha wananchi wa Mtwara, kuonesha kwamba serikali inawasikiliza.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu aliwashirikisha mawaziri Dk. Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara), Dk. Harrison Mwakyembe (Uchukuzi), Prof. Anna Tibaijuka (Ardhi), Dk. Shukuru Kawambwa (Elimu na Mafunzo ya Ufundi), Dk. Mary Nagu (Uwekezaji) na Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani).
Walikuwapo pia viongozi wengine wakubwa wa taasisi za usalama pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Raymond Mbilinyi.
Watendaji hao kila mmoja kwa nafasi yake, alitoa maelezo ya jinsi mikoa ya Kusini itakavyonufaika na fursa za kiuchumi zilizomo katika mipango ya serikali na wawekezaji binafsi.
Taarifa rasmi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, imeeleza kwamba serikali imeahidi kulipa uzito wa kipekee suala la uendelezaji wa Ukanda wa Kiuchumi wa Mtwara (Mtwara Corridor) kama ilivyo kwa Ukanda wa Kilimo wa Nyanda za Juu Kusini Tanzania (SAGCOT).
Waziri Mkuu amenukuliwa akisema kwamba serikali itachukua hatua hiyo ili kuiendeleza kiuchumi mikoa ya Kusini ambayo ni Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Pinda aliwasihi wakazi wa Mtwara kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinaimarishwa kama kweli wanataka mkoa huo uendelezwe.
SOURCE:-TANZANIA DAIMA

Comments