MBUNGE wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR Mageuzi), amesema Serikali inajiandaa kuchakachua mtaala wa elimu inaotarajia kuuwasilisha bungeni Februari 6, mwaka huu.
Katika kutekeleza mkakati huo, amesema ana taarifa za uhakika, kwamba kuna baadhi ya maofisa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wako jijini Dar es Salaam wanataka kubadilisha muhtasari wa mtaala ili uwe mtaala kamili.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, alisema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, tangu Oktoba 30 mwaka jana, alishindwa kuwasilisha mtaala bungeni, badala yake alipiga chenga hadi wakati huu.
“Ni suala la kutia shaka sana, yaani tangu mwaka jana nilipoomba nipewe mtaala wa elimu sikupata hadi leo, lakini Waziri bado anaomba aongezewe siku kana kwamba anakwenda kuuagiza kutoka nje ya nchi.
“Serikali ikae ikijua mtaala wa elimu ni mmoja tu na haupaswi kuwa siri, hawawezi kukaa kikundi cha watu sita au saba wakasema wanaandaa mtaala kinyemela.
“Nasisitiza tena, hatujawahi kuwa na mtaala rasmi Tanzania tangu mwaka 1961, huko walikokaa na kujifungia ili waje na mtaala wa kuchakachua hatutaukubali, tunajua wanataka kutuletea rasimu iliyopo kwamba ndiyo mtaala, ninaitahadharisha Serikali iache kabisa mchezo huo mchafu, wataaibika,” alisema Mbatia.
Huku akionyesha nakala ya rasimu hiyo, alisema Waziri Dk. Kawambwa alilieleza Bunge, kwamba mtaala unaotumika ni wa mwaka 2005, huku rasimu ikionyesha chapa ya kwanza kwa shule za msingi hadi vyuo vya ualimu ni ya mwaka 2012.
“Rasimu ya shule za awali mpaka vyuo vya ualimu iliyoandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania mwaka 2010, na chapa ya kwanza mwaka 2012, inawezekanaje chapa hiyo itoke 2012 wakati tunaambiwa mitaala inayotumika sasa ni ya mwaka 2005?” alihoji na kuendelea:
“Unajua, kinachompa hofu Waziri ni hii chapa ya mwaka 2012, mitaala yote ya elimu ya awali, msingi, sekondari, sekondari kidato cha tano na sita na vyuo vya ualimu, rasimu zote zimechapwa mwaka 2012.
“Sasa waziri atueleze ni kwa nini mtaala wa mwaka 2005 uchapwe mwaka 2012.
“Hali ni tete, tunao ushahidi wa kutosha na ni mwingi, unapofanya ufisadi kwenye elimu ni kuliangamiza taifa, wanaleta mgongano kwenye kanuni ili kulinda uovu.
“Wenyewe mliona siku ile jinsi Naibu Spika alivyomlinda moja kwa moja Waziri, hoja yangu imetengenezwa na kupitiwa na wataalamu wa Ofisi ya Spika, sasa iweje tena waanze kuipindisha na kuitafutia sababu zisizokuwa za msingi.
“Nawaomba Watanzania, kamwe wasikubali maisha yao yachezewe namna hiyo na mimi nawaambia bado sijahitimisha hoja yangu,” alisema Mbatia.
Kwa mujibu wa Mbatia, Serikali inataka kuleta mkanganyiko usiokuwa na maana kwa sababu kiutaratibu, kinachoanza kuandaliwa katika masuala ya elimu ni sera, ikifuatiwa na mtaala na mwisho inafuata rasimu au muhtasari.
Comments
Post a Comment