Katika
mkutano wa Kumi wa Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Spika wa Bunge ndugu Anna Makinda alitangaza mabadiliko kadhaa ya muundo
wa Bunge katika Kamati mbalimbali za Bunge. Moja ya maamuzi ya Spika
yalikuwa ni
kufutwa kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma
ambayo inajulikana kifupi kama POAC. Maamuzi haya yameleta sintofahamu
kwa wananchi wengi na wafuatiliaji wa masuala ya Bunge na Uwajibikaji
katika nchi yetu. Ni muhimu tufahamu uundwaji wa POAC ulitokana na
misingi gani na kwamba Uamuzi wa Spika unarudisha nyuma maendeleo
makubwa ya kujenga Bunge imara na lenye meno. Maamuzi ya Spika ni
kinyume cha kanuni za Bunge, sheria ya Ukaguzi na Katiba ya nchi.
Maamuzi ya Spika yanavuruga Bunge,ni ya hovyo na yanapaswa kupingwa na
kila mdau wa Uwajibikaji nchini.
Baada
ya Tanzania kuingia kwenye zoezi la Ubinafsishaji, mashirika mengi ya
Umma yaliuzwa na mengine kufa kabisa. Wakati huo kulikuwa na chombo
kinaitwa SCOPO (Standing Committee on Parastatal Organisations) kwa
madhumuni ya kusimamia uendeshaji wa Mashirika ya Umma. Bunge lilikuwa
na Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma na kamati hiyo ilifutwa mwaka
1997 kufuatia hatua za ubanifsishaji na ukweli kwamba Mashirika ya Umma
hayatakuwapo na hivyo hapakuwa na haja ya kuwapo kwa kamati hiyo.
Mwenyekiti wa mwisho wa Kamati hiyo alikuwa ni Mzee William Shelukindo
wakati huo akiwa Mbunge wa Jimbo la Bumbuli wilayani Lushoto mkoani
Tanga.
Mwaka
2007, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alifanya mkutano
wa Uwajibikaji na kueleza Taifa kuwa kimsingi Mashirika ya Umma bado
yapo na mahesabu yao, kwa kuwa hayaangaliwi, ni mabaya sana nafedha za
umma zinapotea. Pia alieleza kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ibara ya 143(5) inamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali kutoa taarifa za Ukaguzi za Mashirika ya Umma (Public
Authorities and Other Bodies). Hivyo aliomba Bunge liunde Kamati ya
Bunge ya Mashirika ya Umma ili liweze kupokea, kujadili na kutoa
maelekezo kuhusu mahesabu ya Mashirika ya Umma na kusimamia ufanisi wa
Mashirika ya Umma. Vile vile alishauri Kamati hiyo isimamie sera ya
Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma. Spika wa Bunge wa wakati huo,
kupitia Kamati aliyoiunda chini ya Job Ndugai (wajumbe wengine walikuwa
dkt Willibrod Slaa, Beatrice Shelukindo, Hamad Rashid Mohammed na Nimrod
Mkono) wakaunda Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma kwa mujibu wa
Kanuni za Bunge za Mwaka 2007. Kamati ya POAC iliundwa rasmi mwaka 2008
mwezi Februari. Nilipewa dhamana ya kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Kamati
hii. Sababu za kuanzishwa kwa kamati ya POAC bado zipo na kimsingi
sababu hizo ni za maana sana sasa kuliko ilivyokuwa kabla.
Majukumu
ya POAC yaliainishwa na sehemu ya tatu ya nyongeza ya nane ya Kanuni za
Bunge toleo la mwaka 2007, kanuni ya 115 (13)(a-e). Majukumu hayo ni
pamoja na kushughulikia mahesabu yaliyokaguliwa ya Mashirika ya Umma,
kuainisha maeneo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za Umma, kutathmini
ufanisi wa Mashirika ya Umma na kufuatilia utekelezwaji wa sera ya
ubinafsishaji wa mashirika ya Umma. Kuanzia mwaka 2008 Mdhibiti na
Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali amekuwa akitoa taarifa za
mahesabu ya mashirika kama Katiba ya nchi inavyomtaka na sheria ya
ukaguzi ya mwaka 2008. Sheria hii imeitaja kamati ya POAC kama moja ya
kamati zenye majukumu ya kuwasilisha Bungeni taarifa ya mwaka ya
mahesabu ya Mashirika ya Umma.
Katika
kipindi cha miaka mitano POAC imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa
umahiri na kwa kweli kwa uwazi sana kuliko kamati nyingine zote za
Bunge. Taarifa ya mwisho ya POAC katika Bunge iliyowasilishwa katika
mkutano wa saba wa Bunge, mwezi Aprili mwaka 2012 ulipelekea kutolewa
kwa hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu ambayo ilisababisha
mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri. Hatua hii ilikuwa ni hatua
muhimu sana katika kuweka mizizi ya utamaduni wa uwajibikaji nchini
kwetu. Wakati Kamati inajiandaa na Taarifa yake ya Mwaka 2012 kwenye
Mkutano wa Kumi na Moja, Spika ameivunja. Ikumbukwe maagizo ya mwisho ya
Kamati ya POAC yalikuwa ni kuzuia mifuko ya hifadhi ya jamii kutoa
mikopo kwa Serikali bila ya kuwapo kwa mikataba. Hivi sasa Serikali
imekopa zaidi ya shilingi 1.2 trilioni kutoka mifuko ya Hifadhi ya Jamii
kwa ajili ya miradi mbalimbali, mikopo hiyo ya fedha za wafanyakazi
haina mikataba yeyote na POAC iliona hatari ya fedha za wafanyakazi
kupotea na kuleta madhara makubwa kwa wastaafu nchini.
Katika
maelezo yake Spika amesema nchi nyingine duniani hazina kamati kama ya
POAC. Nadhani waliomshauri Spika waliamua kumdanganya na yeye
akadanganyika. Nchi zote za Afrika Mashariki zina Kamati ya kusimamia
Mashirika ya Umma. Kenya inaitwa Public Investments Committee, Uganda
inaitwa State Corporations Committee na hata nchi nyingine kama India
ambazo zinafuata utamaduni wa kibunge kama wetu wanayo na wanaita Public
undertakings Committee. Nchini Afrika Kusini sio tu kuna Kamati ya
Mashirika ya Umma bali pia kuna Wizara inayosimamia Mashirika ya Umma
(Ministry of Public Entreprises). Kimsingi Kamati ya POAC ilipaswa
kuongezewa nguvu zaidi ili kufikia uwezekaji wa Serikali kwenye
makampuni binafsi badala ya kuifuta. Uwezekaji wa Serikali kwenye
makampuni kama BP, AirTel, Kilombero Sugar, SonGas nk hauna uangalizi
wowote.
Uamuzi
wa Spika wa Bunge kuifuta Kamati ya POAC ni uamuzi unaorudisha nyuma
juhudi za nchi kujenga asasi za uwajibikaji, ni kinyume cha sheria ya
ukaguzi wa umma inayotaja Kamati tatu za Bunge za kusimamia fedha za
Umma na ni kinyume cha Katiba ya nchi. Spika wa Bunge anasema kazi za
Kamati ya POAC zitafanywa na Kamati ya PAC; Tanzania ina jumla ya
Mashirika ya Umma 258 yenye thamani ya shilingi trilioni 10.2 mpaka
mwezi Juni mwaka 2012, hata kamati ya POAC ilikuwa haiwezi kushughulikia
Mashirika yote ya Umma katika mwaka mmoja, PAC itawezaje kusimamia
Wizara za Serikali, Mikoa na wakala za Serikali na wakati huo huo
Mashirika ya Umma 258? Kwa vyovyote vile Taifa linarudi miaka ya kabla
ya 2008 ambapo Mashirika ya Umma yalikuwa kichaka cha kuiba fedha za
Umma. Hivi karibuni Kamati ya POAC iligundua mtindo wa Wizara za
Serikali kupeleka fedha Serikali kwenye Mashirika na kutumia kifisadi
ili kukwepa ukaguzi kwenye Wizara (Wizara ya Utalii ilipeleka zaidi ya
shilingi 600 milioni Bodi ya Utalii mwaka 2010/2011). Ikumbukwe pia wizi
wa EPA, MEREMETA na hata uuzaji holela wa baadhi ya mali za Serikali
kupitia ubinafsishaji ulifanyika nyakati ambazo Bunge halina kamati
inayosimamia Mashirika ya Umma.
Kwa
vyovyote vile Spika wa Bunge amedhihirisha namna ambavyo anafanya
maamuzi bila kuzingatia maslahi ya nchi wala kuzingatia historia ya
uwajibikaji katika nchi. Namna mijadala ya Bunge inavyoendeshwa, namna
anavyobeba ajenda za Serikali katika kujenga Bunge kibogoyo na namna
anavyofanya maamuzi kwa kukurupuka, inahitaji hatua za kuokoa misingi ya
uwajibikaji wa nchi. Ni lazima Spika wa Bunge adhibitiwe kwa kuondolewa
katika nafasi hiyo haraka iwezekanavyo. Spika lazima ajue kwamba
Mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni msimamizi tu wa vikao vya Baraza la
wananchi liitwalo Bunge. Anna Makinda lazima adhibitiwe, vinginevyo
nchi yetu itaumia.
This is amazing, Shocking, Confusing, Itching and really Boaring kwa mtu kama Spika wa Bunge tena mkuu wa muhimili muhimu wa Dola wenye jukumu la msingi la kuiwajibisha serikali. LAZIMA AWAJIBISHWE.
ReplyDelete