
*Asema kisipotekeleza kitaanguka
*Amshangaa Mangula kuhusu rushwa
MWANASIASA mkongwe nchini na muasisi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kingunge Ngombale Mwiru, amekitabiria ushindi chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, iwapo kitatimiza masharti matatu yatakayokiwezesha kushinda.
Amesema upepo wa kisiasa hapa nchini bado unavuma vizuri kwa CCM, hivyo kinapaswa kuchanga karata zake vema ili kujihakikishia ushindi kwa kusahihisha makosa kiliyoyafanya na kujipanga upya.
Kingunge aliyasema hayo juzi, katika mahojiano maalumu na Mtanzania Jumapili, nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine, alichambua mwelekeo wa Taifa, wapi tumekwama, tulikokosea na tuendako.
Akizungumza kuhusu nafasi ya CCM kushinda urais 2015 na nafasi ya chama hicho katika uchaguzi huo, Kingunge aliyataja masharti matatu ambayo alisema kinapaswa kuyatimiza na iwapo kitashindwa, kitaanguka.
Kwa mujibu wa Kingunge, CCM kina nafasi kubwa ya kushinda iwapo kwanza kitawaachia wanachama wake kujitokeza kuwania nafasi za uongozi kwa mujibu wa taratibu za chama.
Sharti la pili alilolitaja ni CCM kiwaachie wanachama waamue bila kuingiliwa juu ya mtu wanayempenda kuwa kiongozi wao na kusisitiza kuwa chaguo la wanachama liheshimiwe na lisiingizwe mizengwe.
Katika sharti lake la tatu, Kingunge alisema katika kipindi cha sasa cha kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa na ule mkuu mwaka 2015, chama kinapaswa kuimarisha utendaji wake wa kazi za chama ndani ya chama.
“Pia kiimarishe utendaji wa kazi za chama nje ya chama ndani ya umma, hususani katika kurejesha uhusiano mwema katika jamii,” alisema Kingunge.
Akizungumza kuhusu makada wa chama hicho walioanza kujipanga kwa ajili ya kugombea urais mwaka 2015, Kingunge alisema kwa mwana CCM kufikiria au kuchangamkia kugombea nafasi ya uongozi, ni haki ya kikatiba hivyo isifanywe kosa, lakini alisisitiza kuwa wakati ukifika wafuate taratibu.
Kauli hiyo ya Kingunge imekuja wakati ambao inatafsiriwa kuwa ni dhambi kwa baadhi ya wana CCM wanaotajwa kuwa tayari wameanza maandalizi ya kuwania urais 2015.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula, amepata kuwaonya makada wa chama hicho ambao wameanza mbio za kuusaka urais katika uchaguzi mkuu ujao, kwamba hawatavumiliwa.
Hata hivyo, Kingunge amesema kwa raia Mtanzania ambaye ametimiza masharti ya kikatiba ana haki na uhuru wa kuwa na matamanio ya kuwa rais au kiongozi yeyote, lakini wakati utakapofika utaratibu ufuatwe.Kuhusu Rushwa ndani ya CCM
Akizungumzia kuhusu rushwa ndani ya CCM, Kingunge amesema hajaona mtu jasiri wa kulisema jambo hilo, huku akipinga staili inayotumika katika kupambana nalo.
Mwanasiasa huyo, ambaye amekitumikia chama kwa muda mrefu na serikali za awamu zote nne, akishika nyadhifa mbalimbali, alisema rushwa ni tatizo la nchi na si la CCM tu, kwamba Taifa lipo katika hali ngumu.
Kingunge amesema CCM imejitahidi sana kupambana na tatizo hilo, lakini imeonekana kushindwa.
“Lazima tukubali CCM imejitahidi sana kukabiliana nalo, pengine tulikosea namna ya kulikabili, rushwa si jambo la taratibu tu, ni suala la itikadi, msimamo wa mtu, imani ya mtu, hivyo suala la maadili…rushwa inatokana na tatizo kubwa la kutokuwa wazalendo,” alisema.
Alisema kwa sababu rushwa ni suala la kimaadili, linahitaji kulikabili kimaadili na apatikane mtu jasiri kweli kweli wa kulizungumza wazi wazi.
“Wajikosoe bila kuoneana aibu kuanzia vikao vya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), wajikosoe jinsi walivyoshiriki vitendo vya rushwa…wapatikane watu jasiri …Watu hao jasiri mimi sijawaona bado, tunataka vikao vitakavyotuambia ukweli,” alisema Kingunge.
Kingunge aliwapiga kijembe baadhi ya wana CCM waliomstari wa mbele katika kupambana na rushwa, akisema kuwa nao ni wala rushwa wakubwa.
Pamoja na hilo, ameshangaa staili inayotumiwa na CCM katika kupambana na rushwa, hasa kupitia kauli mbiu yake ya ‘Vua gamba’.
Amesema kama CCM inataka kupambana na rushwa na matatizo mengine ya nchi, wasiyapunguzie kwa watu wengine.
“Rushwa ni suala la ubinafsi, mtu anataka kupata yeye tu hivyo ananunua watu, sasa unafanyaje kudeal na huo mfumo kwamba walioshinda kwa rushwa unawatoa, je, wale walioshiriki ambao walitoa rushwa na hawakushinda?” alihoji Kingunge.
Alimshangaa Mangula juu ya kauli yake ya kuwapa miezi sita mafisadi ndani ya CCM kuwa wawe wamefungasha virago vyao.
“Sasa rafiki yangu Mangula, nikasema anababaika nini, kila mtu anafahamu kwamba wapo wengi walioshiriki katika rushwa hawakushinda, mnawafanyaje na hawa? Msishughulike na upande mmoja kwa sababu suala hili ni la kimaadili linahitaji kulikabili kimaadili,” alisema Kingunge.Kuhusu CCM kupoteza mvuto
Kuhusu CCM kupoteza mvuto kutokana na kushamiri upinzani nchini, Kingunge alisema chama chao kimejisahau kutokana na kukaa madarakani muda mrefu.
“Tuna matatizo ya kukaa madarakani muda mrefu, sasa mnaweza mkasahau mnapigania nini, mkafikiri mnapigania kuwa madarakani,” alisema Kingunge.
Alisema jamii inavyobadilika mambo nayo yanabadilika, hivyo inahitajika juhudi kubwa ya chama kuendelea kuwa moto moto wa kuyapigania yale ambayo kiliahidia na kwamba kama hakuna jitihada hizo, kulegea kutakuwepo.
Usikose kusoma Mtanzania Jumapili wiki ijayo, Kingunge akichambua kuhusu mambo mbalimbali ya kitaifa, vyama vya upinzani, Bunge nk.
Comments
Post a Comment