
*Yabainika mkataba wake wa kazi umekwisha
*Aendelea kukalia ofisi ya umma isivyo halali
*Yeye ang’aka, asema mkataba wake anaujua JKMSAJILI wa Vyama vya Siasa, John Tendwa anakalia ofisi ya umma kinyume cha sheria, MTANZANIA Jumapili imebaini.
Taarifa za kuaminika zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kwamba kiongozi huyo anaendelea kukalia kiti hicho wakati mkataba wake wa kazi umemalizika.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, Tendwa alipaswa kustaafu mwaka 2010 lakini aliongezewa mkataba wa miaka miwili ambao umemalizika Novemba 2012.
Chanzo hicho kilihoji sababu za kiongozi huyo ambaye ni mlezi wa vyama vya siasa nchini kuendelea kukalia ofisi hiyo licha ya mkataba wake wa nyongeza kumalizika.
Chanzo hicho kilisema Tendwa alipewa mkataba wa miaka miwili ili aweze kusimamia utekelezaji wa Sheria mpya ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 ikizingatiwa kuwa nchi ilikuwa inaingia katika uchaguzi.
“Tendwa alipaswa kustaafu 210, lakini Kikwete (Rais Jakaya Kikwete) akampa mkataba wa miaka miwili aweze kusimamia sheria mpya ya gharama za uchaguzi.
“Mkataba wake umemalizika tangu Novemba mwaka jana lakini bado yupo, mara kwa mara anaenda Ofisi ya Waziri Mkuu ku-lobby (kushawishi) apewe mkataba mwingine,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema Tendwa ameshindwa kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo na sasa anataka apewe mkataba mwingine ili afanikishe mpango wake wa kuendesha vyama vya siasa anavyoona yeye.
“Huo mkataba wa awali hatuoni alichokifanya zaidi ya kuongeza migogoro tu. Hiyo sheria yenyewe ya gharama za uchaguzi hakuna ufanisi wowote ameshindwa kusimamia utekelezaji wake.
“Tunajua kwa nini ana-lobby (anashawishi) anataka kutekeleza mpango wake wa kuendesha vyama vya siasa anavyotaka yeye.
“Tendwa anataka kuvigawa vyama katika madaraja kama vilivyo vilabu vya mpira hiyo uliwahi kuona wapi? Anataka pawepo na vyama vya daraja A, B, C na D.
“Katika jambo la kushangaza, chama chenye alama au daraja D hakitaweza kusimamisha mgombea katika uchaguzi, sasa hiyo kama siyo kuminya demokrasia ni kitu gani?,” kilihoji chanzo hicho.
Alipotafautwa ili kuzungumzia uhalali wa kuendelea kubaki ofisini, Tendwa aling’aka na kusema kuwa suala la mkataba wake aulizwe Rais Jakaya Kikwete kwa kuwa yeye ndiye mamlaka ya uteuzi.
Tendwa alipofuatwa ofisini kwake, alikataa kuzungumzia suala hilo akisema kuwa anachotambua yeye ni kwamba yupo ofisini kwa sheria na majukumu yake yapo kwa sheria.
Hata hivyo, Tendwa alivitaka vyombo vya habari kutoandika wala kujadili suala la mkataba wake kwa vile linaweza kuleta malumbano na hivyo kuhatarisha nafasi yake.
“Ofisi hii ipo hapa kwa mujibu wa sheria na watumishi wake wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria, suala la mkataba wangu kwamba umekwisha au laa mnaweza kumwuliza Rais yeye ndiye aliyeniweka hapa.
“Rais Kikwete ndiye mtu pekee anayeza kujua kama mkataba wangu umekwisha au laa, sitaki malumbano na rais yeye ndiye anayeweza kuniongezea mkataba au vinginevyo.
“Mimi sitaki kulumbana na rais, mambo ya kujibizana kwenye vyombo vya habari hayana maana, mimi nipo ofisini naendelea kufanya kazi,” alisema.
Wakati suala la mkataba wa kazi yake hiyo likiibuka, tayari Tendwa ameingia katika mgogoro na viongozi vyama vya upinzani nchini wakihoji uhusiano wake na chama tawala cha CCM.
Tendwa ameingia katika msuguano huo baada ya kuitaka CCM kusimamisha mgombea wa urais anayekubalika na Watanzania wengi katika uchaguzi wa 2015 kiweze kuhimili nguvu ya upinzani.
SOURCE :MTANZANIA
Comments
Post a Comment