RAIS 2015 NI MWANAMKE!

Banner
  • Sheikh asema atashinda kwa nguvu kubwa
  • Awakata maini Lowassa, Membe, Sitta, Dk. Slaa
MWENYEKITI wa Taasisi ya Kiislamu ya Imamu Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis, amejitokeza hadharani na kutabiri matukio yatakayojiri mwaka huu kuelekea mwaka 2015.


Sheikh Khalifa ambaye ni mmoja wa wanazuoni wa Kiislamu nchini, alisema mwaka 2013 utatawaliwa na mjadala mkubwa kuhusu mrithi wa Rais wa sasa, Jakaya Kikwete ambaye anamaliza muda wake.

Kiongozi huyo wa kidini alisema, upo mpango unaoandaliwa kwa siri wenye lengo la kuwasambaratisha wanasiasa wanaojipanga kuwania urais, ili kumweka katika soko la siasa mwanamke msomi atakayegombea nafasi hiyo.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Sheikh Khalifa alisema mwaka 2013, unatazamiwa kuwa wenye matukio makubwa yakiwamo majanga ya moto, mafuriko na vimbunga vitakavyoleta fazaa kwa watu.

Hata hivyo Sheikh Khalifa, alisema utabiri wake huo unatokana na elimu ya kuambiwa, tofauti na ule uliokuwa ukifanywa na marehemu Sheikh Yahaya Hussein, unaotokana na elimu ya nyota.

Kiongozi huyo alisema iwapo hakutatokea sababu za kuahirishwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ishara zinaonesha kuwa rais ajaye aidha atatokea Kaskazini au Kusini, lakini hatokani na majina ya viongozi wanaotajwa kwa sasa.

Kwa upande wa Kaskazini viongozi wanaotajwa kuwania urais mwaka 2015 ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM) na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), DK. Willbrod Slaa.

Kwa upande wa Kusini anayetajwa kuwania urais ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta (Magharibi).

Wengine wanaotajwa kwa mbali ni Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa zamani wa Hanang’ Frederick Sumaye, anayetoka Kanda ya Kaskazini na Zitto Kabwe (Magharibi).

Kiongozi huyo alikwenda mbali zaidi katika utabiri wake na kusema kuwa, upo mpango unaoandaliwa kwa siri na kundi dogo la viongozi serikalini.

Alisema mpango huo wa siri unalengo la kumuandaa na kumuweka kwenye soko la siasa mwanamke msomi na maarufu, kwa lengo la kumjengea uwezo wa kusimama kugombea nafasi hiyo mwaka 2015.

“Ingawa mpango huo unaonyesha utaundiwa mkakati wa hali ya juu, lakini pia utapingwa kwa kutumia nguvu kubwa sana na endapo utafaulu mwanamke huyo anaweza kuwa ndiye rais ajaye,” alisema.

SOURCE :-MTANZANIA

Comments