*Zitto, Mbatia, Mtanda, CUF wamrarua Muhongo
*January Makamba atoa darasa la utajiri wa gesiUTAJIRI mkubwa wa gesi unaopatikana katika maeneo ya kusini mwa Tanzania unaonekana kuchukua sura na mwelekeo tofauti kadri siku zinavyosonga mbele. Kugundulika kwa gesi katika maeneo hayo ya kusini mwa Tanzania ambako awali kulianza kuonekana kuwa neema ya kitaifa, kidogo kidogo kumeanza kuchukua mweleo wa mzozo unaohusisha viongozi wa serikali, wabunge na watalaamu wa masuala ya nishati.
Katika hatua ya sasa mzozo huo, unaonekana kuchukua sura mpya, siku moja baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kutoa tamko rasmi la serikali juzi.
Waziri Muhongo katika taarifa yake hiyo alisema suala la kusafirishwa kwa gesi kwa njia ya bomba kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam, lilikuwa halikwepeki.
Hatua ya Muhongo kutoa tamko hili imekuja siku chache baada ya wananchi wa Mtwara wanaoungwa mkono na baadhi ya wanasiasa kuandamana kupinga hatua ya serikali kusafirisha gesi kwa njia ya bomba hadi Dar es Salaam.
Miongoni mwa viongozi ambao wamejitokeza na kutoa kauli zao kuhusu sakata hilo la gesi siku moja baada ya Waziri Muhongo kutoa kauli yake ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Tekinolojia, January Makamba, Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Akizungumzia kauli ya Waziri Muhongo, Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alisema kuwa, Profesa Muhongo hakupaswa kutoa majibu mapesi kuhusu sakata hili gumu na lenye maslahi mapana kitaifa.
“Nimesikitishwa na kauli ya Waziri Muhongo, imeonyesha wazi kwamba hii ni dalili ya serikali kuweweseka. Anatoa majibu mepesi katika maswali magumu.
Zitto ambaye amekuwa miongoni mwa wanasiasa wanaoitetea hatua ya wananchi wa Mtwara kuandamana, alisema hoja za serikali zinazojengwa katika muktadha wa kuepuka kile kinachoitwa hofu ya kugawa nchi au kuwashambulia wao kama watu wanaotaka umaarufu wa kisiasa si mpya.
Mwanasiasa huyo alieleza kusikitishwa na hatua ya Waziri Muhongo ya kutaka kuwafanya wananchi wa Mtwara wanaodai haki yao stahiki waonekana kuwa ni watu wasio na shukrani, wachoyo na wenye roho mbaya.
“Kusema watu wa Mtwara na Lindi, hawakuchangia hata kidogo kwenye hazina ya taifa. Hivyo wao kupigia kelele gesi yao ni uchoyo na roho mbaya na kukosa shukurani. Kauli ya Serikali ni kauli ya chombo kinachoendelea kukosa ‘legitimacy’ (uhalali) ya kuongoza taifa.
Alizielezea kauli za Muhongo kuwa ni za mtu aliyekata tamaa na akasema jambo la namna hiyo ni la hatari kubwa kwa Watanzania wa Mtwara waliojitolea damu kulinda uhuru wa nchi yao.
Alisema takwimu za uzalishaji wa korosho, zinaonyesha kuanzia mwaka 1965 mpaka 2011, korosho imeliingizia Taifa fedha kigeni jumla ya dola za Kimarekani bilioni 4.58, hali ya uchumi 2012.
“Serikali inataka kufuta historia ya mchango wa zao la Korosho kwenye uchumi wa nchi yetu kwa sababu ya uroho wa gesi asilia. Kwa nini kauli rasmi ya Serikali haijataja korosho kabisa? Kauli hii, ilipitishwa na ngazi zote za Serikali? Mawaziri wa Serikali wanaotoka mikoa ya Lindi na Mtwara, walikubali kauli kama hii itoke dhidi ya wananchi wao wanaoteseka na zao la korosho miaka nenda miaka rudi?
Alisema Serikali imesahau mchango wa watu wa Lindi na Mtwara katika ulinzi wa Taifa. Alisema moja ya sababu ya mikoa hiyo kuwa nyuma kimaendeleo ni juhudi za ukombozi wa kusini mwa Afrika.
Alisema kambi ya wapigania uhuru wa Msumbiji ilikuwa Nachingwea.
“Kambi ya FRELIMO, iliwekwa kwenye Shamba la Mkonge kilometa 17 tu kutoka mjini Nachingwea ambapo ilikuwa makao makuu ya ukombozi wa Msumbiji.
Alisema hata Rais Samora Machel, Rais Joaqim Chissano na Rais Guebuza, waliendesha mapambano kutoka kusini mwa Tanzania.
Zitto, ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, alisema ni aibu kwa serikali kujitetea kwa kutumia hoja sizizo na ukweli kwa kudai kuwa Dar es Salaam, ni kituo cha kukusanyia mapato ya Serikali.
Alisema watu wazalishaji mali wakubwa katika taifa hili ambao ndiyo wamekuwa wakichangia kiasi kikubwa cha kodi kinachokusanywa Dar es Salaam wako nje ya mkoa huo.
source Mtanzania.
Comments
Post a Comment