MALECELA ANENA YAKE KUHUSU SAKATA LA GESI MKOANI MTWARA

 
WAZIRI Mkuu Mstaafu na Mwanasiasa Mkongwe nchini, John Malecela, ametoa wosia kuhusu mgogoro wa gesi akiiomba Serikali kufanya kila iwezalo ili kuhakikisha kuwa wakazi wa Mtwara wananufaika kwanza na rasilimali hiyo.
Malecela alitoa kauli hiyo jana alipotakiwa na gazeti hili kutoa maoni yake kuhusu mgogoro wa kusafirisha gesi kutoka mkoani Mtwara kwenda jijini Dar es Salaam unaoendelea kushika kasi katika siku za hivi karibuni.
“Ukiwa karibu na waridi unatakiwa kunukia waridi. Wakazi wa Mtwara nao wanatakiwa wanukie waridi,” alisema.
Malecela alisema, pamoja na ukweli kwamba rasilimali inayopatikana nchini ni kwa ajili ya watanzania wote, ukweli kwamba wakazi wa eneo inakopatikana rasiliamali hiyo wanapaswa kunufaika nayo, haukwepeki.
“Hatutakiwi kuwaacha hivi hivi wana-Mtwara eti kwa sababu hii ni rasilimali ya Watanzania wote. Ni lazima wanufaike zaidi, wao kuliko wengine kwa kuwa wako karibu na waridi,” alisema Malecela.
Alisema licha ya gesi hiyo kuwa ya watanzania wote, Serikali inatakiwa kuandaa utaratibu ili kuhakikisha kuwa wananchi wa Mtwara wananufaika zaidi na rasilimali hiyo.
Malecela alieleza kuwa umaskini uliokithiri katika baadhi ya mikoa nchini ukiwamo mkoa wa Mtwara, ndio unaosababisha watu waanze kudai rasilimali zinazotoka katika maeneo yao wakiamini kuwa ndio mwanzo wa ukombozi wao.
“Serikali iyaangalie kwa umakini maeneo yanayotoa utajiri na rasilimali, ni lazima wapewe upendeleo ili wafurahie matunda mali asili yao,” alisema Malecela.


SOURCE:-MWANANCHI

Comments