MZEE YUSUF, AMINI SALMIN WATIFUANA

 

ILIKUWA bado nusu tu, Wakurugenzi wa Bendi za Muziki wa Mwambao nchini, Mzee Yusuf wa Jahazi Modern Taarab na Amini Salmin wa T-Moto, watwangane, Risasi linakupa A-Z.

Mzee Yusuf.
Mtifuano wa wawili hao ulitokea Novemba 3, mwaka huu ndani ya Ukumbi wa Dar Live, Mbagala Zakhem jijini Dar ambako bendi hizo zilikamua kwenye Tamasha la Mitikisiko ya Pwani.
Inadaiwa kuwa, Amini ndiye aliyeanza kumchokoza Mzee Yusuf wakati alipokuwa jukwaani.
Mkurugenzi huyo wa T-Moto alikuwa akilalamikia kitendo cha Jahazi kuimba wimbo wa pili wakati vikundi vilivyotangulia viliimba wimbo mmoja mmoja.
“Wakati Mzee Yusuf alipokuwa akiimba, Amini alikuwa akitoa maneno makali ya kumdhalilisha,” alisema shuhuda huyo.
Inadaiwa kuwa wakati Mzee Yusuf alipokuwa akishuka jukwaani, Amini aliendelea kumkashifu kutokana na mavazi yake ya kung’ara aliyokuwa ameyavaa (angali picha ukurasa wa nyuma).
“Usifikiri wote tuna vichwa vya nyanya wengine tuna vichwa pera,”alisema  Amini na kumfanya Mzee Yusuf kujibu kwa kumwambia:
“Kama wewe una kichwa cha pera wengine tuna vichwa vya nazi.”
Mzee Yusuf alijibu mapigo  zaidi kwa kumwambia Amini aache kuwasumbua watu kwa cheo cha baba yake kwani kama ni urais, alikuwa nao zamani. (Amini ni mtoto wa  Rais Mstaafu wa Zanzibar, Salmin Amour).
“Vita ya maneno kati ya wawili hao vilipamba moto, kila mmoja alionesha kupandwa na jazba, ikafikia hatua wakaanza kukunja mashati ili kutaka kuchapana makonde lakini, wasamaria wema waliingilia kati na kuwatuliza,” kiliongeza chanzo chetu.
Mpaka wawili hao wanaondoka ukumbini hapo, kila mmoja, alikuwa akimponda mwenzake na kudai iko siku watashikishana adabu.
Risasi liliwatafuta wawili  hao na kila mmoja alitoa madai yake.
“Jahazi wamekuwa wakibebwa katika kila idara kuanzia redioni hadi jukwaani, kila bendi iliambiwa ipige wimbo mmoja, T-Moto tukatii hilo bila ya kuongeza hata dakika moja kwa nini Jahazi wacheze rafu? Alihoji Amini.
Kwa upande wake Mzee Yusuf  alisema:” Tulizingatia zaidi usalama tulihofia mashabiki wangeweza kufanya fujo, ilibidi tuchukue uamuzi mgumu wa kutii amri ya mashabiki,” na kudai kuwa kupiga wimbo mmoja au miwili kusingewapunguzia au kuwaongezea chochote katika malipo yao.

Comments