MSHAMBULIAJI mahiri wa Azam FC, Kipre Tchetche, amesema hapendi kuwa mfungaji bora katika Ligi Kuu Bara bali anachoangalia yeye ni kuhakikisha anaiwezesha timu yake kunyakua ubingwa.
Akizungumza na Championi Jumatano, Tchetche alisema anatambua ushindani wa kufukuzia ufungaji bora msimu ni mkubwa lakini hilo halimfanyi akili zake kuzielekeza huko kama watu wengi wanavyofikiri.
“Natambua kuna ushindani mkubwa wa kila mchezaji kupata nafasi ya ufungaji bora wa mabao msimu huu lakini mimi hilo siliangalii kwa sasa ila nataka kuona timu yangu inachukua kombe la ligi na si vinginevyo,” alisema Tchetche.
Tchetche mwenye mabao sita nyuma ya Didier Kavumbagu wa Yanga aliye na mabao saba, alisema akiwa kama mchezaji wa kulipwa atapenda kurudisha fadhila kwa viongozi wa Azam ambao waliona uwezo wake na kuamua kumsajili.
Mchezaji huyo amekuwa akionyesha uhai mkubwa katika kikosi cha timu hiyo inayoshika nafasi ya tatu katika ligi kwa kuwa na pointi 21 na leo inacheza na JKT Oljoro katika Uwanja wa Chamazi, Dar.
Comments
Post a Comment