WAZIRI WA ULINZI: ORODHA YA MAMBO YA MUUNGANO IPUNGUZWE.

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Shamsi Vuai Nahodha amesema Muungano una mambo ambayo Katiba mpya inapaswa ipunguze orodha yake na kubakiwa na manane ili yasimamiwe vizuri.

Nahodha ambaye aliunga mkono mfumo wa Serikali mbili, alisema uwepo wa mambo mengi ndiyo unaoleta mkanganyiko.
Alisema hayo wakati akichangia maoni kuhusu Katiba mpya mbele ya Tume ya kusikiliza Maoni iliyokutana jana na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi mjini hapa.
Katika mkutano huo ambao asilimia kubwa ya wajumbe wote walizungumzia suala la Muungano pekee, Nahodha alipendekeza masuala mengine yote yaondolewa kwenye Muungano ubakiwe na ulinzi, polisi, uraia, mambo ya nje, sarafu, anga na usajili wa vyama vya siasa.
Alisema kwa kuondoa mambo hayo, Bunge la sasa lifanyiwe mabadiliko na liwe na sehemu mbili, ya kwanza itakayozungumzia mambo manane ya Muungano na ya pili izungumzie masuala ya Tanzania Bara.
Aidha, aliendeleza maoni ya kutaka uwepo utaratibu wa kupokezana urais kati ya Bara na Zanzibar kwa kipindi cha kila baada ya miaka ya 10.
“Wengine tunapoeleza hivyo wanapata wasiwasi wanadhani tunataka kupata rais substandard (chini ya viwango),” alisema Nahodha na kusisitiza kwamba vigezo na sifa viwe vile vile kama vilivyopo.
Kuhusu mgawanyo wa mapato, alisema suala hilo limebaki kuwa la kutupiana mpira kutokana na tatizo kwamba halikuwekwa kwenye Katiba.
Waziri huyo aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), alipendekeza Zanzibar ipewe asilimia 15 ya mapato ya vyanzo vyote vilivyo kwenye Muungano na itajwe kwenye Katiba.
“Mwanzo waliangalia idadi ya watu kwamba uwiano wa watu wa Zanzibar ni 3.5 wakasema mapato ya Zanzibar ni kama asilimia nne,” alisema na kusisitiza kwamba vigezo hivyo si sahihi kwa kuwa Serikali ina jukumu sawa na bara la kuhudumia watu wake.
Nahodha ambaye alisema Zanzibar imepoteza mamlaka yake ikiwa ni pamoja na kupoteza uwezo wa kupata misaada kutoka nje ikiwemo OIC, aliendelea kusema, “Zanzibar ilipounda Muungano tumepoteza mamlaka ya kushirikiana na nchi za nje… hivyo hiyo asilimia 15 ni sawa na kulipwa fidia,” alisema.
Wengine waliochangia ni Mwakilishi wa Chumbuni, Machano Othman Said (CCM) alipendekeza Muungano uliopo uendelee, lakini akataka katika Katiba ijayo, Rais wa Zanzibar awe Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Mwakilishi wa Jimbo la Chonga, Abdalah Juma Abdalah (CUF) alipendekeza mfumo wa Muungano wa mkataba maalumu chini ya utaratibu maalumu ambao kila upande unakuwa huru kupunguza jambo litakaloonekana halina maslahi kwake.
Naye Mwakilishi wa Tumbe, Rufai Said Rufai (CUF) pamoja na kupendekeza Zanzibar na Tanganyika kila moja iwe na mamlaka yake kamili kwa lengo la kuunda Muungano wa mkataba, alitaka Wabara wanaoishi visiwani na Wazanzibari walioko Bara, wawe na hiari ya kuishi wanakotaka bila kubughudhiwa.

Comments