
Waziri huyo, Mathias Chikawe anayeiongoza
Wizara ya Katiba na Sheria, ameshindwa katika uchaguzi wa nafasi ya
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) katika wilaya ya Nachingwea,
mkoani Lindi.
Kuanguka kwa Chikawe kumethibitishwa na
Katibu wa CCM Mkoa wa Lindi, Adelina Gefi alipozungumza na gazeti hili
jana kwa njia ya simu.
Alisema nafasi ya Mjumbe wa NEC kutoka
Nachingwea imekwenda kwa kijana mwenye umri wa miaka 24, Fadhili Liwaka
aliyevuna kura 795 dhidi ya 561 alizopata Chikawe ambaye kwa sasa ana
umri wa miaka 61, huku mshindani mwingine katika nafasi hiyo, Lowama
Mtonya (43) alipata kura 13 tu.
Hata hivyo, habari ambazo gazeti hili
ilizipata zinasema kuwa, mshindi wa nafasi hiyo alikimbizwa hospitali
mara baada ya matokeo, kutokana na kuanguka katika ukumbi wa mkutano na
kupoteza fahamu jana jioni.
Amelazwa katika Hospitali ya Ndanda
wilayani Masasi. Chanzo chetu cha habari kinasema kuwa, baada ya
kuanguka na kuzimia kwa muda alizinduka na kumwambia baba yake mzazi,
amwakilishe katika kuhesabu kura na yeye kukimbizwa hospitalini.
Wakati wengi wakipigwa butwaa na matokeo
hayo, juzi wajumbe wa mkutano huo walimchagua Mkuu wa zamani wa wilaya,
Albert Mnali kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM wilaya ya Nachingwea.
Mnali aliyejizolea umaarufu kutokana na
msimamo wa kuwacharaza bakora walimu wa shule za msingi wilayani Bukoba,
mkoani Kagera kutokana na kile kilichodaiwa uzembe uliosababisha
wanafunzi kufeli, msimamo uliomponza na kujikuta akivuliwa madaraka na
kufukuzwa kazi na Rais Jakaya Kikwete Februari 2009.
Katika uchaguzi wa juzi, Mnali ambaye
mwaka 2010 alijaribu kuwania ubunge, lakini jina lake likaishia katika
mchujo wa ndani ya chama, aliibuka mshindi wa nafasi ya uenyekiti baada
ya kupata kura 948. Fadhili Mkuti alipata kura 251 na Mohammed Kamlo
aliambulia kura 79.
Gefi aliongeza kuwa, katika uchaguzi
wilayani Ruangwa, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia elimu, Kassim Majaliwa
aliwabwaga wapinzani wake katika ujumbe wa NEC baada ya kupata ushindi
wa kura 578, huku Kalembo Napenya akiambulia kura (254) na Namkumbya
Hassan (250).
Aidha, katika nafasi ya uenyekiti wa CCM
wilayani hapo, Njinjo Mussa alishinda kwa kupata kura 704 huku wapinzani
wake ambao ni Adelfina Joseph (174) na Selemani Mmuya (324).
Katika wilaya ya Lindi Vijijini, Mbunge
wa Mchinga, Said Mtanda alishinda nafasi ya ujumbe wa NEC kwa kupata
kura 1,066 huku wapinzani wake ambao ni Mikidadi Alawi wakiambulia kura
277 na Shaibu Buriyani (276) kati ya kura 1,196.
Gefi alisema katika wilaya hiyo nafasi ya
mwenyekiti wa CCM wilaya ilienda kwa Mohammed Nyangamara aliyeshinda
kwa kupata kura 535 huku wapinzani wake Masudi Chitende (246) na
Athumani Hongonyoko (415).
Kwa upande wa wilaya ya Kilwa, nafasi ya
uenyekiti wilaya ilinyakuliwa na Yusufu Kopakopa aliyepata kura 873 huku
wenzake ambao ni Ally Mngindo akiambulia (452) na Mikidadi Kinogeandaga
(271) kati ya kura 1,566 zilizopigwa.
Nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya
Taifa katika wilaya hiyo ilichukuliwa na Balozi Ally Mchumo aliyepata
kura 1,113 na wakati Njuma Ibrahim alipata kura (56) na Saidi Mkunga
(435).
Katibu huyo wa CCM mkoa wa Lindi pia
alithibitisha ushindi wa mke wa Rais, Salma Kikwete katika ujumbe wa NEC
kwa wilaya ya Lindi Mjini, baada kupita bila kupingwa.
Aidha alisema nafasi ya uenyekiti wa
wilaya hiyo ya Lindi, ilichukuliwa na Muhsin Ismail aliyepata kura (476)
huku wapinzani wake ambao ni Abdallah Livembe wakiambulia kura 138 na
Manyanya Nasibu (38) kati ya kura 655 zilizopigwa wilayani hapo.
Nyalandu apeta Singida Mkutano Mkuu wa
uchaguzi CCM wilaya ya Singida vijijini, umemchagua Naibu Waziri wa
maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya
Taifa (NEC) kupitia wilaya hiyo. Nyalandu, ambaye pia ni Mbunge wa
Singida Kaskazini, alipata nafasi hiyo baada ya kukomba kura 897 kati ya
jumla ya kura 1,157 zilizopigwa.
Mpinzani wake wa karibu, Dafi Bulali aliambulia kura 131, Manase Sabasaba alipata kura 102 na Juma Mwiru kura 27 tu.
Naye Justin Monko, mkuu wa wilaya ya
Singida Queen Mlozi, Amani Nyekele, Rehema Majii na Aziza Kiduda
walichaguliwa kuwa wajumbe wa Mkutano mkuu wa Taifa.
Narumba Banarbas, ambaye alikuwa anatetea
nafasi yake ya mwenyekiti wilaya CCM alifanikiwa kufanya hivyo baada ya
kupata kura 607 ambapo Mwiru Juma alipata kura 480.
Kwa mujibu wa Msimamizi wa Uchaguzi huo,
Moses Matonya, washindi wa nafasi ya ujumbe wa halmashauri kuu wilaya
kundi la vijana ni Manase Sabasaba, Jumanne Salum, Daud Elias na Hilda
Lazaro Wajumbe wa halmashauri wilaya kupitia kundi la wanawake ni Amina
Mweri, Hilda Lazaro, Neema Matiti na Zuena Mohammed wakati nafasi za
wajumbe wa halmashauri kuu kundi la wazazi ni Justin Monko, Edward
Yaredi, Ilanda na Ramadhani Mangu.
Katika uchaguzi uliofanyika wilayani
Ikungi, Mkandarasi mashuhuri wa majengo mkoani hapa, Hassani Tati
alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo kwa kishindo.
Tati alichukua nafasi hiyo kwa kupata
kura 968 dhidi ya washindani wenzake wawili, Bwaba Mpaki Ibrahimu
aliyepata kura 211 na Athuman Magwe aliyepata kura 89. Naye Jonathan
Njau ambaye alinyang’anywa nafasi ya ubunge na Tundu Lissu wakati wa
Uchaguzi mkuu mwaka 2010, safari hii alichaguliwa kwa kishindo na
mkutano huu kuwa mjumbe wa NEC kupitia wilaya hiyo.
Njau alifanikiwa kupata kura 775 na hivyo
kuwabwaga vibaya washindani wenza Hamisi Ngila na Mkhotya Moris. Nafasi
ya mkutano mkuu taifa waliochaguliwa kuwakilisha wilaya ni pamoja na
mkuu wa wilaya ya Kishapu, Wilson Nkhambaku, Theresia Nkuhi, Mkuu wa
wilaya ya Ikungi Manju Msambya, mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya
Singida, Celestine Yunde na Samwel Gabriel Dinawi.
Kutoka UVCCM ni Paulo Hema (732) na
Reuben Elisha Abraham (671) na UWT ni Amina Omari Munjori (774) na Amina
Mdandau (654). Halima Mlacha Dar na Abby Nkungu, Singida
Comments
Post a Comment