VURUGU ALIYEDHIHAKI MSAHAFU: CHANZO NI SIMU


MTOTO anayedaiwa kudhihaki kwa kukikojolea kitabu kitakatifu cha Quran (jina linahifadhiwa) ameponzwa na ujumbe wa simu uliosambazwa jijini Dar na kulifanya tukio hilo kuwa kubwa zaidi.
Watu waliounasa ujumbe huo wamesema kuwa mara baada ya kutokea kwa tukio hilo, baadhi ya Waislamu wa Mbagala jijini Dar, walianza kuwataarifu wenzao wanaoishi katika vitongoji mbalimbali kwa kutumia SMS.


Baada ya kupata taarifa hizo, Waislamu walianza kulizungumzia tukio hilo misikitini Ijumaa iliyopita na kukusanyana kwenda Mbagala kwa ajili ya kumsaka mtoto huyo.
Habari zaidi zinasema kuwa mtoto aliyekidhihaki kitabu hicho aliponzwa na tambo zake kuwa hakuna kitakachomtokea baada ya kufanya kitendo hicho.

Kwa mujibu wa shuhuda mmoja, kabla mtoto huyo hajafanya tukio hilo, kulitokea mabishano kati ya watoto wenye imani tofauti za kidini.
Hali hiyo ilitokea baada ya watoto hao ambao wanasoma Shule ya Sekondari ya Chamazi na kuishi jirani walipokutana na yule wa Kiislamu akiwa amebeba msahafu.

Baada ya kukutana kukatokea mabishano kati yao huku yule wa Kikristo akisema kitabu kile kilikuwa ni majini na yule wa Kiislamu akikitetea.
“Mtoto wa Kiislamu alimkanya mwenzake kwamba asikichezee kitabu kile kwani anaweza kugeuka nyoka, ndipo mwenzake alipokichukua na kukimwagia mkojo, kisha kukitemea mate,” alisema jirani huyo.

Jirani huyo aliendelea kubainisha kuwa baada ya tukio lile, mtoto wa Kiislamu alirudi nyumbani kwao na ‘kuuchuna’ huku mwenzake akijitapa mitaani kwamba ameweza kukikojolea kitabu kile na hakupata madhara.

Baadhi ya watu wazima waliposikia tambo hizo za kijana huyo wa Kikristo, waliamua kwenda kumuuliza yule kijana wa Kiislamu kama ni kweli mtoto yule alifanya kitendo cha kukikojolea kitabu chao na mtafaruku mkubwa ukaanzia hapo

Mpaka gazeti hili linaenda mitamboni, mali kadhaa yakiwemo makanisa na magari yalikuwa yamevunjwa na imeripotiwa kuwa jenereta moja kubwa la umeme la Kanisa la Sabato limeibwa na baadhi ya watu hao waliokasirishwa na kitendo kilichofanywa na mtoto huyo.

Comments