
Release No. 167
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Oktoba 12, 2012
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Oktoba 12, 2012
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom inaendelea
kesho (Oktoba 13 mwaka huu) kwa timu kumi kupambana kwenye viwanja
vitano tofauti katika raundi ya saba ya ligi hiyo yenye timu 14.
Polisi
Morogoro itaikaribisha Azam kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro
wakati mwamuzi wa FIFA, Oden Mbaga atakuwa Uwanja wa Kumbukumbu ya
Sokoine jijini Mbeya kuchezesha mechi kati ya wenyeji Tanzania Prisons
na Oljoro JKT.Jijini Tanga, Simba itakuwa mgeni wa Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Simon Mberwa kutoka Pwani akisaidiwa na Godfrey Kihwili na Abdallah Uhako wote kutoka Arusha.
Mechi nyingine za kesho ni Ruvu Shooting dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi, na Mtibwa Sugar watacheza na Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
Wakati huo huo, Azam imeomba mechi zake za nyumbani dhidi ya Yanga na Simba zichezwe kwenye uwanja wake wa Azam Complex ulioko Chamazi badala ya Uwanja wa Taifa.
Nayo Ruvu Shooting imeomba mechi yake ya ugenini dhidi ya Yanga ya Oktoba 20 mwaka huu ichezwe Uwanja wa Taifa badala ya Uwanja wa Azam Complex.
Maombi hayo yatawasilishwa kwenye kikao cha Kamati ya Ligi ya TFF kinachotarajiwa kufanyika kesho (Oktoba 13 mwaka huu) kwa ajili ya kufanyiwa uamuzi.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Comments
Post a Comment