SIMBA KUKAMATA BASI LA YANGA SAKATA LA MBUYU TWITE

UONGOZI wa Simba umesema iwapo mahasimu wao, Yanga,
hawatawalipa fedha wanazodai kutokana na sakata la usajili wa beki Mbuyu Twite, raia wa Congo, watatinga mahakamani kupata kibali cha kulikamata basi lao ili kufidia fedha hizo.
Hivi karibuni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia kwa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, liliitaka Yanga iilipe Simba dola 30,000 ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 45 za Kitanzania, inazomdai mchezaji huyo ambaye alizipokea baada ya kukubali kuichezea timu hiyo lakini baadaye akatimkia Jangwani.
 Akizungumza na Championi Jumatatu, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alisema hadi sasa hawajapokea kiasi chochote cha fedha kutoka kwa Yanga licha ya kubaki siku chake katika siku 21 walizopewa na TFF ili kumalizana.
“Tunasubiri, iwapo hatutapewa fedha zetu ndani ya muda uliopangwa na TFF, basi tutalazimika kwenda mahakamani ili kuweza kuomba kibali cha kukamata basi lao ili waweze kutupatia fedha zetu.
“Hadi sasa bado hatujazipata fedha hizo na hatujapata taarifa yoyote kutoka kwao na hatujui chochote kinachoendelea, hivyo tunasubiri siku zifike ili tuweze kukabidhiwa fedha hizo,” alisema Rage.
Kwa upande wa Yanga, alipofuatwa Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga, kuzungumzia fedha hizo, alisema mchakato bado unaendelea na watawalipa wakati wowote kwa kuwa muda wa siku 21 waliopewa na TFF bado haujaisha.

Comments