SHOMARI KAPOMBE HATI HATI KUIKOSA KAGERA SUGAR LEO

BEKI wa mabingwa wa soka wa Ligi Kuu Bara, Simba, Shomari Kapombe, ataukosa mchezo wa ligi hiyo dhidi ya Kagera Sugar leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, kutokana na kuendelea kuugulia maumivu ya kifundo cha mguu.

Kapombe alipata maumivu hayo wakati wa mchezo dhidi ya Yanga Oktoba 3, mwaka huu, baada ya kukanyagwa na mshambuliaji Said Bahanuzi.
Akizungumza na Championi Jumatano, Kapombe ambaye alishindwa kufanya mazoezi juzi, alisema alitonesha kifundo hicho wakati wa mechi dhidi ya Coastal Union, iliyochezwa Jumamosi iliyopita.
“Kifundo nilitonesha kwenye mechi dhidi ya Coastal Jumamosi wakati nataka kupiga mpira, nikakwaruza chini, ndiyo nikawa nimetonesha.
“Sijajua kama nitacheza kwenye mechi ya Kagera kwa kuwa daktari hajaniambia, lakini najua hata nisipocheza timu itafanya vyema bila mimi, kwa kuwa tuna wachezaji wengi wazuri,” alisema Kapombe.
Hata hivyo, daktari wa Simba Cosmas Kapinga alisema kuwa hatima ya mchezaji huyo ingejulikana jana jioni baada ya kufanyiwa vipimo kwenye Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam.

Comments