SERGIO AGUERO AWALALAMIKIA WAAMUZI KUWAPENDELEA WACHEZA WA UINGEREZA

Sergio AgueroSergio Aguero anaamini wachezaji raia wa Uingereza hupendelewa na waamuzi, wakilinganishwa na wenzao kutoka ng'ambo.
Mchezaji huyo wa klabu ya Manchester City, na mwenye umri wa miaka 24, alifunga bao la kusawazisha, katika mechi ambayo timu yake iliishinda Fulham magoli 2-1.
Wenzake kutoka Argentina, Pablo Zabaleta na Carlos Tevez, licha ya kudai penalti, maombi yao yalikataliwa na mwamuzi.

Alipoulizwa ikiwa anadhani wachezaji wa kigeni hukabiliwa na changamoto zaidi ikilinganishwa na wachezaji wenye asili ya Uingereza, alijibu: "Ndio, kila wakati. Hutokea kila mahali.

"Kuna hali ya kuwapendelea wachezaji wanaotoka nchi hiyo."
Alipoulizwa ikiwa anadhani waamuzi huwa wamo katika hali ya kuwashuku wachezaji wa kigeni, Aguero alijibu:"Naam, pengine. Ni jambo linaweza kutokea, lakini sidhani hapa hilo linafanyika.

"Ikiwa linafanyika, halitamfaa yeyote.

"Hapa nchini England kuna wachezaji wengi wa kigeni, karibu idadi sawa na Waingereza, na sio sawa kwa wengine kupendelewa zaidi ya wenzao."

Mchezaji huyo wa Argentina alikubaliana na meneja Roberto Mancini kwamba Fulham hawakufaa kupata penalti, kufuatia Zabaleta kumtega John Arne Rise, nafasi ambayo aliitumia Mladen Petric katika kuiwezesha timu ya Fulham kupata bao la kutangulia katika mechi hiyo.

Comments