
Akiongelea ishu hiyo ya Refa, Ofisa
Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema kuwa Akrama alichezesha Mechi
ya Jumapili ya Yanga na African Lyon ambayo Yanga walishinda bao 3-1 na
wanashangaa leo tena ameteuliwa kwenye Mechi ya Simba na Yanga.
Hata hivyo, Kamwaga alifafanua: “Hili
limetushangaza sana, lakini hatuna tatizo ila tunamtaka achezeshe kwa
kufuata haki maana ile mechi kuna watu wanaweza kufa kwa presha, wengine
wameweka rehani nyumba zao na vitu mbalimbali hivyo si mchezo wa utani.
Tunamsihi afuate sheria hatutaki apendelee timu ya aina yoyote, sisi
tunataka matokeo ya uwanjani kama tukifungwa na yeye amechezesha vizuri
tutakuwa wa kwanza kumpongeza.“
Mara ya mwisho kwa Yanga na Simba
kukutana ilikuwa ni Mei 6 Mwaka huu katika Mechi ya mwisho ya Msimu wa
2011/12 ambayo Simba iliicharaza Yanga bao 5-0 na kutawazwa rasmi
Mabingwa wa Tanzania Bara.
Pia, kipigo hicho ndicho kiliangusha
himaya ya Uongozi wa Yanga wa Mwenyekiti Lloyd Nchunga na kupelekea
kufanyika Uchaguzi mdogo uliomsimika Mfadhili mkuu wa Klabu hiyo, Yusuf
Manji, kuwa ndio Mwenyekiti mpya.
Kwa sasa, tangu Ligi Msimu huu ianze,
Simba imekuwa na matokeo mazuri kwa kushinda Mechi zao zote 4 na wapo
kileleni wakiwa na Pointi 12 wakati Yanga wameanza kwa kusuasua ikiwa na
Pointi 7, ikiwa nafasi ya 6, kwa kushinda Mechi mbili, kufungwa moja na
kutoka sare moja.
Matokeo hayo yameifanya Yanga imtimue
Kocha wao Tom Saintfiet na kumwajiri Mholanzi Ernie Brandts aliewasili
Nchini Ijumaa iliyopita lakini kwa sasa jukumu la kuifundisha Yanga
limekuwa chini ya aliewahi kuwa Mchezaji wao mahiri Fred Felix Minziro.
Simba, chini ya Kocha Mkuu Mserbia
Milovan Cirkovic, itatinga Uwanjani bila Nyota wao wawili, Emmanuel Okwi
na Amir Maftah, ambao wanatumikia Vifungo baada ya kulimwa Kadi
Nyekundu hivi karibuni.
Hata hivyo, Simba bado inao Wachezaji
wakali, wakiongozwa na Kipa mkongwe Juma Kaseja, ambao ni kina Felix
Sunzu toka Zambia, Mghana Daniel Akuffor, Mrisho Ngassa , Chipukizi
Edward Christopher, Mwinyi Kazimoto na Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
Nao Yanga inao Wachezaji wa kutisha kina
Hamisi Kiiza toka Uganda, Mrundi Didier Kavumbagu, Said Bahanunzi,
Simon Msuva, Athumani Idd ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Frank Domayo,
Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ pamoja na Mbuyu Twite.
VIKOSI VINATARAJIWA:
Yanga: Yaw Berko, Mbuyu
Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Athuman
Idd ‘Chuji’, Frank Domayo, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbagu, Hamisi
Kiiza, Simon Msuva.
Simba: Juma Kaseja,
Nassoro Masoud, Paul Ngalema, Juma Nyosso, Shomari Kapombe, Jonas Mkude,
Mwinyi, Kazimoto, Amri Kiemba, Felix Sunzu, Edrward Christopher, Mrisho
Ngassa.
VIINGILIO:
Kiingilio cha chini ni sh. 5,000 kwa
viti vya rangi ya kijani ambavyo ni 19,648 kwenye uwanja huo wenye uwezo
wa kuchukua watazamaji 60,000. Watazamaji watakaoketi kwenye viti vya
rangi ya bluu ambavyo ni 17,045 watalipa sh. 7,000 kwa tiketi moja.
Sh. 10,000 ni kwa viti vya rangi ya
chungwa ambavyo viko 11,897 wakati VIP C inayochukua watazamaji 4,060
itakuwa sh. 15,000. Kwa upande wa VIP B tiketi ni sh. 20,000 na VIP A
yenye watazamaji 748 tu kiingilio kitakuwa sh. 30,000.
WAAMUZI:
Refa: Mathew Akrama kutoka Mwanza
Refa Wasaidizi: Samuel Mpenzu kutoka Arusha, Ephrony Ndissa wa Dar es Salaam
Refa wa Akiba: Oden Mbaga wa Dar es Salaam.
Comments
Post a Comment