MAKONGORO NYERERE NAYE APIGWA CHINI UWENYEKITI CCM MKOANI MARA

Makongoro NyerereMWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Mara, Makongoro Nyerere amefuata njia waliyopita wenyeviti wenzake, John Guninita wa Dar es Salaam, William Kusilla wa Dodoma na Petro Kingu wa Morogoro, baada ya kushindwa kutetea kiti chake katika uchaguzi uliofanyika juzi mjini Musoma.

Katika uchaguzi huo wa CCM unaoendelea, umewashuhudia Kusilla akibwagwa na Mbunge wa Afrika Mashariki, Adam Kimbisa mkoani Dodoma, Guninita akishindwa kufua dafu kwa Ramadhan Madabida kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Kingu akipigwa mwereka na Mbunge Innocent Kalogeries huku Mussa Shekimweri akishindwa kufurukuta kwa Mbunge wa Lushoto, Henry Shekifu mkoani Tanga.
Hata hivyo, wakati hao wakianguka, wenzao Khamis Mgeja wa Shinyanga, Onesmo Nangole wa Arusha, Lukas Ole Mukusi wa Manyara na Hassan Wakasuvi wa Tabora wametetea nafasi zao.
Makongoro ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye jana Taifa liliomboleza miaka 13 tangu kifo chake, ameshindwa kwa kubwagwa na Christopher Sanya.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi uliofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Wasichana ya Songe Manispaa ya Musoma, Msimamizi wa uchaguzi huo, Nazir Karamagi alimtangaza Sanya kuwa mshindi baada ya kupata kura 481 na Makongoro ambaye pia ni Mbunge wa Afrika Mashariki, alipata kura 422.
Uchaguzi huo ulirudiwa katika nafasi ya Mwenyekiti baada ya mshindi wa awali kushindwa kuvuka nusu ya kura ambapo katika uchaguzi wa mwanzo, Sanya alipata kura 500, Makongoro kura 371 na Enock Chambiri kura 140; matokeo yaliyosababisha kura kurudiwa kwa wagombea wawili.
Aidha, Katibu wa Fedha na Uchumi alichaguliwa Marwa Mathayo aliyepata kura 49 na mpinzani wake, Dk Sema alipata kura 6; wakati mwandishi mkongwe wa habari, Maxmillian Ngesi alishinda nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi, kwa kura 25, akiwashinda Godwin Kumila aliyepata kura 17 na Ibrahim Kazi kura 9.
Mkoani Tabora, Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Hassan Wakasuvi ameshinda tena kiti hicho kwa miaka mitano ijayo baada kuwashinda wagombea watatu; Zuberi Mwamba, Juma Nkumba na Haji Bagio.
Hata hivyo, Nkumba aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Mkoa kabla ya Wakasuvi, alitangaza kujitoa kabla ya kupigiwa kura kama ilivyokuwa kwa Bagio.
Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi wa Uchaguzi huo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya NEC Taifa, Mwigulu Mchemba alisema katika uchaguzi huo kura zilizopigwa ni 996, ambapo Wakasuvi alipata kura 921 na mshindani wake, Mwamba alipata kura 75 na kura zilizoharibika ni 16.
Mkoani Geita, Mkutano Mkuu wa kwanza wa CCM mkoani humo, umemchagua Joseph Msukuma kupata ushindi wa kishindo dhidi ya wapinzani wake wawili, hivyo kuingia kwenye rekodi ya kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho katika Mkoa mpya wa Geita.
Amechaguliwa ikiwa ni takribani miezi 10 tangu ang'olewe kwenye nafasi ya uenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita na madiwani wenzake kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka.
Msukuma alipata kura 565, kati ya 698 ikiwa ni ushindi wa zaidi ya asilimia 80 ya kura zote zilizopigwa katika uchaguzi huo uliozishirikisha wilaya tano za Nyang'hwale, Geita, Chato, Mbogwe na Bukombe.
Alifuatiwa na Jeremiah Ikangala aliyepata kura 130 ikiwa ni asilimia 18, huku aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo, John Luhemeja akipata kura 5 kati ya kura 698.
Mkoani Manyara, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Lukas Ole Mukusi ameibuka kidedea tena huku wapinzani wake wawili wakiomba kujitoa hata kabla ya kupigiwa kura.
Msimamizi wa Uchaguzi huo, Mjumbe wa NEC, Christopher ole Sendeka aliwataja walioomba majina yao yaondolewe ni Issa Katuga na Godwin Nagoli, ingawa walijitoa walipata kura 18 na mwingine kura 19.
Ole Sendeka alisema Mukusi alipata kura 629 na kura zilizopigwa ni 693, zilizoharibika ni 27 na kura halali ni 669.
Mkoani Dar es Salaam, wagombea waliobwagwa katika uchaguzi huo uliofanyika juzi ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa huo, John Guninita aliyepata kura 214 na mwanasiasa mkongwe wa chama hicho, Mattson Chizii kura 52 wakati mshindi alikuwa Ramadhani Madabida aliyepata kura 310.
Naye Guninita aliyepata upinzani mkubwa kutoka kwa Madabida hadi kunyang’anywa kiti hicho, alikubali matokeo ya kushindwa kwake huku akisisitiza kuwa demokrasia ilitawala.
Nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha ilichukuliwa na Abbas Tarimba aliyepata kura 35 na kuwabwaga Eugine Mwaiposa ambaye ni Mbunge wa Ukonga aliyepata kura 12 na Michael Wambura kura mbili.
Aidha, katika nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi ilichukuliwa na Juma Simba ‘Gaddafi’ aliyepata kura 40 na kumbwaga mtoto wa Waziri Mkuu mstaafu John Malecela, William Malecela aliyepata kura tisa.
Mkoani Tanga, Mwenyekiti wa zamani Mussa Shekimweri amepigwa mwereka na Mbunge wa Lushoto, Henry Shekifu katika uchaguzi uliofanyika juzi katika Chuo cha Eckenford mjini humo.
Kwa mujibu wa Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga, Gustav Muba, mbali ya Shekimweri, mgombea mwingine wa uenyekiti aliyeshindwa ni Mathew Kuziwa, katika uchaguzi uliosimamiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dk Abdallah Kigoda.
Muba alimtaja mshindi wa nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi ni Mathew Mganga aliyemshinda Sadiki Kallaghe huku Mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani maarufu Profesa Maji Marefu akitetea kiti chake cha Katibu wa Fedha na Uchumi dhidi ya Hamis Msumari na Ngoda.
Akihutubia Taifa jana mkoani Shinyanga katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru na Kumbukumbu ya miaka 13 ya kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete aliwapongeza Mgeja na mwenzake wa Simiyu, Dk Titus Kamani.
“Hongereni sana, najua kazi haikuwa rahisi, kule pwani kuna msemo bahari kuu huvukwa, hongereni sana,” alisema Rais Kikwete.

Comments