MAASKOFU NAO WAJAJUU, WAITAKA SERIKALI IWACHUKULIE HATUA WALIOFANYA FUJO MAKANISANI

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Valentino MokiwaMAASKOFU wa Kanisa la Anglikana Tanzania wameitaka Serikali kuwachukulia hatua za kisheria waumini wa Kiislamu waliofanya fujo kuharibu baadhi ya makanisa likiwamo la Anglikana la Roho Mtakatifu lililoko jijini Dar es Salaam.

Kauli ya maaskofu hao 22 ilitolewa jana jijini Mwanza na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Valentino Mokiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari.
“Tunalaani, tumeshtuka kwa vile sio mara ya kwanza kutokea hapa nchini. Katika siku za hivi karibuni, kumetokea matukio kama hayo Zanzibar na Bagamoyo, ambako makanisa yaliharibiwa na kuchomwa moto na baadhi ya waumini wa dini hiyo kwa sababu wanazozijua wao,” alisema.
Askofu Mokiwa alisema hawajawahi kusikia watu waliohusika na uharibifu wa majengo ya ibada na mali za Kanisa wamechukuliwa hatua stahili na Serikali, ikiwamo kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa Sheria.
“Tunajiuliza kwa nini hilo halikutokea Zanzibar wala Bagamoyo, tunaanza kufikiri kuwa huenda Serikali inawaogopa au kuwalinda waumini hao wanaoutumia mwavuli wa dini yao kuharibu majengo ya makanisa na mali zilizoko kwenye makanisa hayo."
Alimshukuru Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum kwa jinsi alivyoelewa mgogoro huo na kuuelezea kupitia vyombo vya habari juu ya chanzo kuwa ni ubishi, ushindani wa barabarani wa watoto wawili wa shule.
CCM yalaani Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema wanalaani vurugu, udhalilishwaji wa dini na uharibifu wa nyumba za ibada vilivyofanyika Mbagala na kuvitaka vyombo vya Dola viwachukulie hatua za kisheria wahusika.
Katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) lililochomwa, jana waumini wake walitakiwa kutolipiza kisasi kwa mtu yeyote, wala kumchukia kwa kuchoma moto na kuharibu Kanisa na kuwataka kuombea amani ya nchi.
Akihubiri katika Ibada KKKT Usharika wa Mbagala, Kaimu Katibu Mkuu, Theolojia, Misioni na Uinjilisiti Mchungaji Boniface Kombo alisema pamoja na huzuni waliyoipata kutokana na uharibifu huo, ni vema kuwaombea rehema wahusika na si kuomba laana maana maandiko hayaruhusu kufanya hivyo.
“Kuna watu wanasema upole wenu (Wakristo) ndio unaowagharimu, lakini sisi tunasema upole wetu una faida kwa Mungu, hata mjinga akinyamaza anaonekana ana hekima. Hii si vita yetu ni ya Mungu, Mungu, anajua kushughulika nao,” alisema Mchungaji Kombo.
Kutokana na uharibifu uliofanyika juzi, mamia ya waumini wa kanisa hilo walilazimika kufanya ibada nje ya kanisa hilo.
Awali, akitoa salaam za Jimbo Kuu la Kusini Diyosisi ya Mashariki na Pwani, Mkuu wa jimbo hilo, Amani Lymo alisema Kanisa lina imani na uongozi wa Rais Jakaya Kikwete kuwa atalishughulikia suala hili kwa umakini.
Kwa upande wake, Rais Jakaya Kikwete amewataka viongozi wa dini nchini kutochukua uamuzi wakiwa na hasira kutokana na tukio la vurugu na uharibifu wa nyumba za ibada lililotokea Mbagala jijini Dar es Salaam kwa kuwa kuna hatari ya kufanya makosa.
“Narudia kusema, jana (juzi) katika ziara yangu niliwasihi viongozi wa dini na wananchi wajiepusha na jazba na kulipiza kisasi, niliwashauri wasifanye uamuzi wakiwa na hasira kwani wanaweza kutoa maamuzi yenye makosa,” alisema Rais Kikwete akihutubia Taifa jana katika kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru mkoani Shinyanga

Comments