IMEELEZWA
kuwa vurugu za kikundi cha Waislamu zilizotokea Mbagala hivi karibuni
ni matokeo ya muda mrefu ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete kupuuzia kushughulikia matatizo yao.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na wajumbe wa Kamati
Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mabere Marando na
Profesa Abdallah Safari, wakati wakizungumza na waandishi wa habari juu
ya msimamo wa chama hicho dhidi ya vurugu za kidini zilizotikisa Jiji la
Dar es Salaam wiki hii.
Marando alisema kuwakamata viongozi wa Kiislamu pasipo
kushughulikia matatizo yao si njia sahihi kwani kuna hatari ya kuzalisha
Waislamu wengi wenye msimamo mkali dhidi ya serikali na kuifanya nchi
kutotawalika.
“Kabla ya uhuru Waislamu walikuwa na taasisi zao serikali ya TANU,
kwa ajili ya kulinda masilahi yake ikavifutilia mbali na kuamua
kuwawekea Waislamu Bakwata na kutunga sheria za kuongoza, nataka mtambue
matatizo ya Waislamu wote hayasimamiwi na Bakwata, waitwe Waislamu na
waulizwe shida zao,” alisema Marando.
Aliongeza kuwa kabla ya uhuru Waislamu walipambana kwa kuamini
walikuwa wakinyanyaswa na kwamba baada ya uhuru hawakuona mabadiliko
yoyote, hivyo wanalazimika kujitafutia uhuru mwingine mbali na ule wa
kutoka katika mikono ya wakoloni.
Alisema serikali isisubiri vifo vitokee ndiyo ione umuhimu wa
kushughulikia matatizo hayo na badala yake ijipe muda wa kukaa na
makundi yote kutafuta muafaka.
“Siamini kama kuna tatizo baina ya Waislamu na Wakristo bali mfumo
wa serikali unawalazimisha Waislamu kuamini hivyo kwa kuwa wametengwa,
hawasikilizwi hawathaminiwi na sasa wako kama yatima kwanini?” alihoji
Marando.
Akizungumzia utekwaji wa watu unaoendelea nchini, Marando alisema
serikali haiwezi kukwepa lawama hizo na kwamba matamshi ya viongozi wa
Ikulu kuwa hawamfahamu Ramadhani Ighondu ni hadaa kwa Watanzania.
“Sheikh Farid alipotea katika mazingira ya ajabu na hili ni jukumu
la serikali kujua hatima ya raia wake lakini leo tunaona vyombo vya
ulinzi vikisema havihusiki wala havina habari na kupotea kwake, haya ni
majibu kama yale yale yaliyotolewa kwa Dk. Ulimboka,” aliongeza Marando.
Kwa upande wake Profesa Safari alizungumzia kitendo cha Jeshi la
Wananchi wa Tanzania kuingilia kati kutuliza ghasia inaonesha kuwa
serikali imeshindwa kuongoza nchi kwa kufuata sheria.
“Jeshi la Wananchi limefuata nini mtaani? Kuna tishio gani la amani
inayowalazimisha wao kuingia mtaani? Kwa kuwa tunafahamu suala la
kutangaza hali ya hatari na jeshi kuingia mtaani lazima liwe na baraka
ya Bunge,” alisema Safari.
Aliongeza kuwa mara nyingi serikali imeshauriwa kutatua migogoro
baina ya Waislamu na serikali, lakini ushauri huo umekuwa ukipuuzwa.
Comments
Post a Comment