HAIJAWAHI KUTOKEO TZ

Vurugu zenye sura ya kiimani, zilizotikisa Kitongoji cha Mbagala, Dar na kuibua mtafaruku baada ya mwanaharakati wa Kiislam, Sheikh Ponda Issa Ponda kukamatwa kwa madai ya uchochezi na sintofahamu ya Uamsho inayoinyuka Zanzibar, kwa pamoja vimetajwa kuwa mtaji kwa imani ya ki-Freemason huku ikidaiwa ni vurugu kubwa za kwanza kutokea nchini.

Waislam na Wakristo ulimwenguni kote, hivi sasa wanatakiwa kuwa macho kwa sababu kuna madai kwamba, imani hiyo kupitia jamii yake ya siri, yaani Illuminati, inaendesha njama hatari kuhakikisha dini hizo zinatoweka.
Kutokana na angalizo hilo, wajuzi wa mambo ya Freemason wameeleza kuwa inapozuka migogoro ya kiimani kama ilivyo sasa nchini, mamlaka za jamii hiyo ya siri hufanya juu chini kuhakikisha muafaka haupatikani ili mnyukano uendelee.
“Freemason wamedhamiria kuitawala dunia. Adui mkubwa wa Freemason ni Uislam na Ukristo, kwa hiyo wamekuwa wakifanya jitihada kubwa kuhakikisha waumini wa dini hizo wanagombana,” alisema Mifsud Carlos, aliyedai amewahi kufanya kazi kwenye moja ya mahekalu ya imani hiyo nchini Uingereza.

Mifsud alisema: “Katika kipindi hiki, usishangae zikaibuka chokochoko hata kwa upande wa Wakristo. Hizo ni njama za watu hao wenye uchu wa kuitawala dunia.”
Tangu wiki iliyopita, taifa liliingia  kwenye hekaheka za machafuko, hatari ikianzia Mbagala ambako mtoto Emanuel Mwinuka, 13, alidaiwa kukojolea Msahafu, hivyo kuwakasirisha watu waliodai ni Waislam ambao waliharibu makanisa na mali nyingine.
Jumatano na Alhamisi wiki hii, Waislam waliandamana kwenda Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar, wakishinikiza Ponda aachiwe huru, baada ya kukamatwa, akituhumiwa kufanya uchochezi.


Wakati hali ikiwa hivyo Dar es Salaam, Zanzibar mambo yalikuwa mabaya zaidi, watu wanaodaiwa ni wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho, walifunga mitaa kwa saa kadhaa, wakachoma matairi na baadhi ya majengo, wakishinikiza kuachiwa huru kwa kiongozi wao, Sheikh Farid, waliyedai ametekwa na polisi.
Hata hivyo, mnajimu aliye pia mtaalamu wa mambo yanayohusu jamii ya Freemason, Maalim Hassan Yahya alisema: “Siamini sana Freemason kuhusika, migogoro iliyopo sasa ina sura ya majini. Kuna majini yanayotaka damu imwagike.”
Kumbukumbu zinaonesha kuwa vurugu zinazodaiwa ni za kidini zilizotokea hivi karibuni nchini ni za kwanza kwa ukubwa tangu uhuru wa Desemba 9, 1961.


Wakati huohuo, Sheikh Ponda na wenzake 49, juzi walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na kusomewa mashtaka manne ya kufanya vurugu, kula njama za kutenda kosa, kujimilikisha ardhi kinyume na sheria, wizi na kuingia kwa nguvu eneo lisiloruhusiwa.
Washtakiwa wote wamenyimwa dhamana na kurudishwa mahabusu hadi Novemba Mosi, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo. Ulinzi uliimarishwa mahakamani hapo huku kukishuhudiwa kuwepo kwa magari ya maji ya kuwasha na askari wengi wa vikosi vya ulinzi na usalama waliokuwa na silaha.

Comments