BABA AMUONDOA MWANAE (KIPA) DAR YOUNG AFRICAN

BABA Mzazi wa kipa wa Yanga, Mohamed Said, amemtaka mwanaye, Said Mohamed, asiendelee kuichezea timu hiyo kwa kuwa amekuwa akiwekwa benchi kwenye kila mchezo.
Mohamed, tangu ajiunge na Yanga Juni, 2011 ameshindwa kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo kutokana na ushindani uliopo, kukiwa na makipa wengine kama Yaw Berko na Ally Mustapha ‘Barthez’.
Kwa mujibu wa rafiki wa karibu wa kipa huyo, baba wa mlinda mlango huyo alitoa tamko hilo wiki iliyopita kutokana na mwanaye kuwekwa benchi akiwa na uwezo mkubwa.
Chanzo hicho kilisema mzazi huyo analishutumu benchi la ufundi la Yanga kwamba lina malengo mabaya ya kutaka kushusha kiwango cha mwanaye.
“Uwezekano wa Said kuendelea kuichezea Yanga ni mgumu kutokana na baba yake mzazi kukasirishwa na kitendo cha mwanaye kukaa benchi wakati ana kiwango kikubwa cha kudaka.
“Baba yake anataka kumuondoa katika dirisha dogo au msimu ujao na kumpeleka Coastal Union ambayo imeonyesha nia ya kumsajili kwa muda mrefu,” kilisema chanzo hicho.
Alipoulizwa kuhusiana na hilo, Said alisema: “Hizo taarifa ni za kweli kabisa, hivi karibuni baba alinipigia simu na kuniuliza sababu ya mimi kutocheza nikamuelezea, lakini kikubwa amenishauri niondoke na niende kwenye timu itakayonipatia nafasi ya kucheza kuliko kuendelea kuua kipaji changu Yanga.”

Comments