ASKOFU MKUU WA KANISA LA ANGLIKANA (MOKIWA) ATOA CHOZI HADHARANI


 Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana nchini, Dk Valentino Mokiwa.

 ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kianglikana nchini, Dk Valentino Mokiwa aliwapa nyuso za huzuni waumini wake baada ya kutoa chozi kuwalilia wananchi wa mikoa ya kusini kutokana na kuharibika vibaya kwa Barabara ya Kibiti- Lindi.
Dk. Mokiwa alijikuta akitoa chozi hadharani baada ya kusafiri kwa gari na kujionea ubovu wa barabara hiyo alipokuwa anakwenda kwenye sherehe ya miaka 100 ya Kanisa la Nanyindwa, wilayani Masasi hivi karibuni.
“Nawalilia wananchi wa mikoa ya kusini. Angalieni barabara ya kwenda Arusha, Mbeya, Dodoma nakadhalika zinapitika, kwa nini hii ya kusini ni mbovu kiasi hiki,” alisema Askofu Mokiwa wakati akitoa hutuba kanisani humo.
Huku akiwaangalia baadhi ya waumini waliokuwa ndani ya kanisa hilo waliowahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, akiwemo Kate Kamba, Mkuvia Maita na Dk. Msamati, kiongozi huyo wa kiroho aliwataka viongozi hao kukutana na vigogo wa serikali ili kuondoa adha ya barabara hiyo ya kusini.
Awali kiongozi huyo alilizindua kanisa hilo la Nanyindwa lililokarabatiwa linaloongozwa na Padri wa Mtaa, Frederick Hokororo na sherehe hiyo ilihudhuriwa na Askofu wa Dayosisi ya Masasi, Patrick Mwachiko, Askofu wa Jimbo la Njombe, John Mwela  na wa Newala, Askofu Oscar Mnung’a pamoja na mapadri 13.
Barabara ya Kibiti-Lindi imekwama kwisha tangu Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ang’atuke madarakani mwaka 2005 ambapo kutoka Kijiji Cha Nyang’wale hadi Nchinga (zaidi ya kilomita 80) haijaisha na ipo katika hali mbaya.

Comments