AKUFFOR AWAPIGA AZAM BAO LA MITA 20 JANA CHAMAZI

MSHAMBULIAJI wa Simba raia wa Ghana, Daniel Akuffor, ameifungia timu yake bao maridadi lililofanya kocha wake, Milovan Cirkovic, ashinde na furaha siku nzima ya jana.
Akuffor amekuwa akihaha kuhakikisha anarudisha uwezo wake wa kufumania nyavu katika mechi za Ligi Kuu Bara akiwa ameshafunga bao moja hadi sasa.
Mshambuliaji huyo alifunga bao hilo jana katika mechi ya kirafiki dhidi ya Azam FC, maalum kwa nyota wa timu hizo ambao wamekuwa wakikosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar, Mghana huyo alifunga bao la umbali wa mita 20 na kuisaidia Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.
Mabao mengine ya Wekundu hao yalifungwa na Uhuru Suleiman na Ramadhan Singano ‘Messi’ huku yale ya Azam yakifungwa na Khamis Mcha na Zahoro Pazzi.
Bao hilo la Akuffor lilimfurahisha sana Milovan ambaye alimtaka mshambuliaji huyo afanye hivyo hata kwenye mechi za ligi.
“Nimefurahi kuona hata katika michezo ya kirafiki timu yangu inashinda, lakini pia nimeridhishwa na kiwango cha wachezaji wangu ambao wamekuwa wakikosa kuanza katika michezo ya ligi na leo (jana) wameonyesha kwamba bado wapo sawa.
“Tumepata mabao mazuri lakini ukiniuliza ni bao lipi limenivutia zaidi, nitakwambia ni lile la Akuffor ambalo linafungwa na nyota wachache wenye uwezo duniani,” alisema Milovan.

Comments