Skip to main content
WALIMU NCHINI KENYA NAO WAANZA MGOMO
Maelfu ya walimu nchini Kenya wameanza mgomo wao rasmi wakidai kuwa
serikali imekuwa ikipuuza kilio chao kuongezwa mishahara kwa miaka
mingi.
Walimu hao ni wa shule za misingi na zile za upili na leo
wamesusia kazi wakitaka nyongeza ya mishahara huku shule nyingi nchini
humo zikiathirika.
Walimu hao wamekiuka agizo la mahakama
lililoharamisha mgomo huo. Shule nyingi katika miji mikubwa mfano
Mombasa, Nairobi na Nakuru zilisalia kufungwa.
Walimu hao wanadai nyongeza ya kati ya asilimia miamoja na miatatu.
Walimu wa shule za upili pamoja na wahadhiri wa vyuo vikuu wamesema watajiunga na mgomo huo baadaye wiki hii.
Mgomo
huu unajiri wakati shule zikifungua kwa muhula wa tatu kitu ambacho
walimu hao wanasema sio hoja kwani wamekuwa wakigoma kila muhula wa tatu
unapofungua kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita wakidai hiyo nyongeza.
Wanasema
kuwa serikali haina usawa katika mishahara kwa wafanyakazi wa sekta ya
umma kwani ni hivi maajuzi tu wauguzi na wafanyakazi wengine wa umma
walipoongezwa mishara baada ya kugoma. Wanadai kuwa walimu wamepuuzwa.
Mgomo huu umeonekana kufanikiwa kwani shule nyingi zimesalia kuwa bila walimu wanafunzi wengi wakibaki nyumbani.
Walikuwa
wamebeba mabango yenye ujumbe kwa serikali kuwa wao hawawezi kula panya
kwa mishahara midogo ambayo wanapata. Na vile vile walisema kuwa
wamechoka na ahadi za uongo za serikali.
Mgomo huo uliitishwa na mashirika ya wafanyakazi yanayowakilisha takriban walimu laki mbili na nusu.
Wameahidi kuendelea na mgomo hadi matakwa yao yatakapotimizwa.
Comments
Post a Comment