Skip to main content
WAISLAMU WOTE WALIOKAMATWA KUACHILIWA KWA DHAMANA
Yaagiza Waislamu wote waliozira kuhesabiwa waachiwe kwa dhamana�ukamataji usitishwe.
Kamanda wa Kanda Maalum Suleiman Kova akiwatuliza
waumini wa kiislam waliokuwa na jaziba nje ya ofisi ya Wizara ya Mambo
ya Ndani ya nchi baada ya kuandamana ili kupeleka malalamiko ya kuhusu
waislamu waliokamatwa kwa kukaidi kujiandikisha sensana kuwataka
serikali wa waachie mara moja wote.
Serikali jana
imesalimu amri kwa kuwaagiza Makamanda wa Polisi wote nchini kuwaachia
kwa dhamana waumini wa dini ya Kiislamu waliokuwa wanashikiliwa na Jeshi
la Polisi kwa tuhuma za kukataa kushiriki kwenye zoezi la Sensa ya Watu
na Makazi linalomalizika rasmi leo nchini.
Aidha, imealiagiza jeshi hilo kusitisha ukamataji wa watu kutokana na zoezi hilo.
Tamko lililotolewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ,
Mbarak Abdulwakil, kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo ambaye yuko nje
nchi kikazi, liliagiza Waislamu hao wanaoshikiliwa kuachiwa kwa masharti
ya dhamana baada ya majadiliano na viongozi wa Kiislamu.
Hii inafuatia maelfu ya Waislamu kutoka Jumuiya na Taasisi za Kiislamu
Tanzania, jana kuvamia majengo ya ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la
Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kushinikiza kuachiwa huru
kwa wenzao waliokamatwa katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na
Zanzibar kwa sababu ya kukataa kuhesabiwa katika zoezi hilo.
Tamko hilo lililosomwa mbele ya Waislamu hao pia lilieleza kuwa mambo
mengine yaliyotajwa kwenye risala ya Waislamu yatashughulikiwa mara
baada ya Waziri mwenye dhamana na Naibu wake kurejea nchini.
Waumini hao wanawake kwa wanaume, walianza kumiminika katika maeneo hayo
kwa nyakati tofauti kwa mafungu, kuanzia saa 7.30 mchana, baada ya
Swala ya Ijumaa, wakitokea katika misikiti mbalimbali ya jijini Dar es
Salaam na vitongoji vyake.
Waliongozwa na Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda na Sheikh Rajabu Katimba.
Kuanzia muda huo, barabara nyingi zilifungwa kupisha makundi ya waumini
hao waliokuwa wakiandamana kwa amani kwenda katika maeneo hayo, huku
wakipaza sauti kwa kutamka: “Takbiyr, Allaahu Akbar’, “Laa ilaaha
Illallah.”
Baada ya kufika, walikusanyika nje ya majengo ya ofisi hizo na kuanza
kuhamasishana pamoja na mambo mengine, kupinga hatua ya kukamatwa kwa
wenzao.
Wakati hayo yakiendelea, waumini hao waliokuwa watulivu, walitumia
wawakilishi wao wanne kwenda kuwasilisha risala yenye madai yao kwa
uongozi wa wizara na Jeshi la Polisi.
Viongozi wa waumini hao waliokwenda kuonana na viongozi wa wizara pamoja
na Jeshi la Polisi, ni pamoja na Amiri wa Umoja wa Wahadhiri wa
Kiislamu Tanzania, Sheikh Kondo Juma Bungo na Amiri wa Jumuiya ya
Wanafunzi wa Kiislamu Tanzania (Tamsiya), Jafari Mneke.
Wengine ni Imamu Mkuu wa Msikiti wa Mtambani, Kinondoni, jijini Dar es
Salaam, Sheikh Suleiman Abdallah na Mdhamini wa Taasisi ya Almallid,
mzee Amani Mushi.
Kwa mujibu wa Sheikh Kondo, wakiwa katika ofisi hizo, walikutana na
kuzungumza na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mbaraka Abdulwakil, pamoja na
maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi Makao Makuu na Kanda Maalum ya Dar
es Salaam.
Alisema mazungumzo yao yaliyochukua zaidi ya saa tatu, yalifikia tamati
baada ya Katibu Mkuu huyo kukubali kwa maandishi kwamba, Waislamu wote
waliokamatwa kwa sababu ya kukataa kuhesabiwa katika sensa wataachiwa
huru bila masharti yoyote.
Sheikh Kondo alisema Katibu Mkuu huyo pia alikubali kwamba, hakuna
muumini yeyote atakayekamatwa tena kwa sababu ya kukataa kuhesabiwa
katika sensa.
Alisema katika maandishi hayo, Abdulwakil aliahidi kuwa atawaagiza
makamanda wa polisi wa mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar
kuhakikisha wanaagiza mara moja kuachiwa huru kwa Waislamu wote
waliokamatwa na kushikiliwa kwa sababu hizo.
Awali, akisoma risala hiyo katika kikao hicho, Mneke alisema wanalaani
vitendo vyote alivyoviita vya ‘unyama’ na ‘unyanyasaji’ alivyodai kuwa
vimekuwa vikifanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya Waislamu na kutaka
vikomeshwe mara moja.
Alisema wanapinga vitendo hivyo kwa kuwa wanaamini vinakwenda kinyume cha haki za raia na haki za binadamu.
Waislamu kupitia jumuiya na taasisi zao, wamekuwa wakipendekeza mambo
matatu yatekelezwe katika sensa; ikiwamo kipengele cha dini kirejeshwe
katika dodoso la sensa.
Mapendekezo mengine, ni kuwapo wawakilishi wa dini zote katika
ukusanyaji wa takwimu na majumuisho na kuundwa tume huru ya sensa.
Kwa mujibu wa Mneke, mapendekezo hayo waliyasilisha serikalini sambamba
na kutoa msimamo wa Waislamu kwamba, hawatawakabili watendaji wa sensa
kuwazuia kufanya kazi yao wakati wa zoezi la sensa.
Pia Waislamu hasa walio chini ya Umoja wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania hawatashiriki sensa ya watu na makazi.
Hata hivyo, serikali kupitia Rais Jakaya Kikwete, ilitoa tamko la kutokukubaliana na mapendekezo hayo ya Waislamu.
Risala hiyo ilisomwa pia mbele ya umati wa waumini waliokusanyika katika maeneo hayo.
Baada ya wawakilishi wa Waislamu kurejea, walitoa taarifa kwa umati wa
waumini waliofurika nje ya majengo ya ofisi hizo juu ya kilichojiri na
mwafaka uliofikiwa katika kikao hicho kati yao na ujumbe wa wizara na
Jeshi la Polisi.
Baada ya kupokea taarifa hizo, wauminin hao walilipuka kwa kupaza sauti
kali za “Takbiyr, Allahu Akbar” na kuanza kuondoka katika eneo hilo kwa
maandamano ya amani.
Walipita katika Barabara za Bibi Titi Mohamed na Morogoro na kwenda moja
kwa moja hadi katika Msikiti wa Kichangani, Magomeni, ambako pamoja na
mambo mengine, walipeana taarifa zaidi kuhusiana na mustakabali wa haki
na maslahi yao kama Waislamu.
Hata hivyo, Waislamu hao wamesema wanatarajia kufanya maandamano mengine
katika siku watakayoitaja, kwenda Baraza la Mitihani la Taifa (Necta)
ya kumng’oa Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza hilo Dk. Joyce Ndalichako.
Comments
Post a Comment