Skip to main content
TAKRIBANI WATU 32 WAUAWA KATIKA MAPAMBANO SUDAN
Jeshi la Sudan na waasi wanasema wamekuwa katika mapambao tofauti mara mbili yaliyowaacha watu kadhaa kuuawa.
Jeshi linasema limewaua wapiganaji 32
walioshambulia kijiji magharibi mwa eneo la Darfur wakati waasi nao
wakidai kuwa wamevitimua vikosi vya serikali kutoka eneo hilo.
Katika
tukio tofauti Khartoum inasema kuwa waasi 45 wameuawa katika kijiji cha
eneo la kusini la Kordofan, karibu na mpaka wa kusini wa Sudan.
Waasi wa Vuguvugu la Haki na Usawa (The Justice
and Equality Movement-JEM) wamesema wamekiteka kijiji hicho huku wakiua
askari mmoja.
Mwaka jana vikundi vya waasi katika majimbo
mawili na pia katika jimbo la Blue Nile walianzisha muungano wenye lengo
la kuiondoa serikali ya rais Omar al-Bashir.
Khartum inaishutumu Sudan Kusini kuwaunga mkono waasi hao.
Serikali mjini Juba inakanusha shutuma hizo ikiilaumu serikali ya Sudan kuyaunga mkono makundi ya waasi Sudan Kusini.
Mapigano ya hivi sasa yanakuja wakati Marekani
ikiwa imetoa onyo kuhusu mgogoro unaoendelea wa mpaka kati ya Sudan na
Sudan Kusini.
Onyo hilo lilitolewa na balozi wa Marekani
katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice kufuatia mkutano wa Baraza la
Usalama kujadii mgogoro huo.
Sudan Kusini imekubali pendekezo la suluhu ya mpaka lililotolewa na Umoja wa Afrika, lakini Sudan inakataa pendekezo hilo.
Tarehe ya mwisho ya Agosti 2 ya kufikia muafaka iliyokuwa imewekwa na Umoja wa Mataifa imeshindwa kuzaa matunda.
Hata hivyo pande zote mbili zinashinikizwa kuwa zimefikia makubaliano kabla ya tarehe mpya iliyowekwa ya Septemba 22.
Sudan na Sudan Kusini zimekuwa katika mgogoro kuhusu mpaka kati ya nchi hizo mbili na mapato ya uchimbaji mafuta.
Sudan Kusini ilipata uhuru kutoka Sudan mwaka
jana, ikimaliza miaka mingi ya mapigano kati ya eneo la kaskazini
linalokaliwa na Waislamu wengi na lile la kusini lenye Wakristo wengi na
dini nyingine.
Comments
Post a Comment