CHINA YAAHIDI KUKUZA UCHUMI ZAIDI

Rais Hu Jintao wa Uchina ameahidi kuendelea kukuza uchumi wa nchi yake, ili kusaidia kufufua uchumi wa dunia. Uchumi wa Uchina ni wa pili kwa ukubwa duniani.Bwana Hu aliahidi kwenye mkutano wa viongozi wa nchi za Jumuia ya Asia-Pacific, unaofanyika mjini Vladivostok Urusi, kwamba Uchina itafuata sera za kupangilia na itajaribu kuzidisha soko la ndani ya nchi. Amesema pia kuwa mataifa yote ya eneo hilo nayo yana jukumu la kuendeleza amani na utulivu.

"Mabibi na Mabwana, uchumi wa dunia uko katika hali tete, na kazi muhimu sasa, ni kufumbua matatizo na kufanikiwa kuchangamsha uchumi ili uendelee kukua.
Kuendeleza shime na utulivu pamoja na kukuza uchumi katika eneo la Pacific ni kwa maslahi ya nchi zote za kanda hii, na pia ni jukumu letu sote." Alisema.

Naye Waziri Mkuu wa Australia, Julia Gillard, ilibidi aondoke kwenye mkutano huo kurejea nyumbani, kwa sababu amefiwa na baba yake, John Gillard, aliyekuwa na umri wa miaka 93.

Comments