
Yanga v Simba Oktoba 3, marudiano Siku ya mwisho Ligi 18 Mei 2013!
NGAO ya JAMII Simba v Azam Septemba 11
WACHEZAJI 17 WAPINGWA KWENYE USAJILI!!
Hatimae Shirikisho la Soka Tanzania,
TFF, leo limetoa Ratiba ya Ligi Kuu Bara inayodhaminiwa na Vodacom na
Ligi hii itaanza Septemba 15 lakini hapo Septemba 11 ni pambano la
fungua pazia Msimu mpya kugombea Ngao ya Jamii kati ya Mabingwa Simba na
Timu ya iliyomaliza nafasi ya pili Azam FC itakayochezwa Uwanja wa
Taifa Jijini Dar es Salaam.
RATIBA=Mechi za Ufunguzi.
Septemba 15
Simba v African Lyon [Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam]
Polisi Morogoro v Mtibwa Sugar [Jamuhuri Morogoro]
Tanzania Prisons v Yanga Sokoine Mbeya]
Mgambo JKT v Coastal Union [Mkwakwani Tanga]
JKT Ruvu v Ruvu Shootings [Azam Complex Dar es Salaam]
Kagera Sugar v Azam [Kaitaba Kagera]
Toto Africans V JKT Oljoro [CCM Kirumba Mwanza]
FAHAMU: RATIBA KAMILI ya MZUNGUKO wa KWANZA Septemba 11 hadi Novemba 11 Bofya http://www.telelablogsport.com
TAARIFA KAMILI TOKA TFF:
Release No. 139
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Agosti 31, 2012
MTIHANI WA MAWAKALA WA WACHEZAJI SEPT 27
Mtihani kwa ajili ya watu wanaotaka kuwa
mawakala wa wachezaji wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la
Mpira wa Miguu (FIFA) utafanyika Septemba 27 mwaka huu saa 4 kamili
asubuhi ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kwa wanaotaka uwakala huo wanatakiwa
kujisajili ambapo watapewa kanuni mbalimbali za FIFA na TFF ili waweze
kujiandaa kikamilifu kwa mtihani huo utakaokuwa na sehemu mbili. Sehemu
ya kwanza ni maswali kutoka FIFA wakati nyingine ni kutoka TFF. Ada ya
mtihani ni dola 50 za Marekani.
Pia Damas Ndumbaro na Ally Mleh wa
Manyara Sports Management ambao tayari ni mawakala wanaotambuliwa na
FIFA wanatakiwa kufanya mtihani huo kama wanataka kuendelea na uwakala
kwa vile muda wa leseni zao za awali umemalizika.
Mawakala wengine ambao ni John Ndumbaro, Mehdi Remtulla, Ally Saleh, Yusuf Bakhresa na Said Tully leseni zao bado ziko hai.
WACHEZAJI 17 WAPINGWA KWENYE USAJILI
Klabu mbalimbali zimewasilisha pingamizi
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupinga usajili wa
wachezaji 17 walioombewa usajili katika timu za Ligi Kuu.
Toto Africans ya Mwanza imewawekea
pingamizi wachezaji Enyinna Darlinton aliyeombewa usajili Kagera Sugar,
na Mohamed Soud anayekwenda Coastal Union kwa maelezo kuwa bado ina
mikataba na wachezaji hao.
Pia Flamingo ya Arusha inapinga usajili
wa wachezaji wake Kelvin Friday Iddy katika timu za Azam na Salim Walii
(Polisi Mara) kwa vile taratibu za kuwahamisha bado hazijafanywa. Nayo
Kagera Sugar inapinga usajili wa beki David Charles Luhende kwenda Yanga
kwa vile ada ya uhamisho haijalipwa.
Super Falcon ya Chanjamjawiri,
Chakechake, Pemba inapinga wachezaji wake wanne; Edward Christopher
Shija, Samir Said Luhava (Simba), Robert Joseph Mkhotya (African Lyon)
na Sultan Juma Shija (Coastal Union) kusajiliwa katika timu hizo kwa
maelezo taratibu halali za uhamisho hazikufuatwa.
Mchezaji Othman Hassan aliyeombewa
usajili Coastal Union anapingwa na Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba
na timu hiyo unaomalizika Mei 24, 2013. Nayo Rollingstone Multipurpose
Ateclass Foundation ya Arusha inapinga usajili wa Kigi Makassy kutoka
Yanga kwenda Simba hadi itakapolipwa fidia ya kumlea mchezaji huyo kwa
vile bado hajafikisha umri wa miaka 23.
Azam inapinga usajili wa Ramadhan Chombo
‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo bado ina mkataba naye unaomalizika
Juni 11 mwakani. Nayo Simba inapinga Kelvin Yondani kusajiliwa Yanga kwa
maelezo kuwa ina mkataba naye uliosainiwa Desemba 23 mwaka jana.
Vilevile Simba imewasilisha malalamiko
ya mchezo usio wa kiungwana katika usajili wa Mbuyu Twite aliyeko Yanga
kwa maelezo alisaini mkataba na klabu yao Agosti Mosi mwaka huu mbele
yao, viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) na APR
ambapo alilipwa dola 30,000 na nyingine 2,000 ikiwa ni fedha ya kujikimu
na nauli yake ya kujiunga na klabu hiyo.
Nayo Yanga inapinga Simba kuwaacha
wachezaji Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiyavanga na Lino Masombo
kwa maelezo walishapatiwa leseni za kucheza Ligi ya Tanzania
walizozitumia kwenye mashindano ya Kombe la Kagame. Pia inapinga
Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga Simba kwa vile ana leseni ya kuchezea
Azam kwa msimu wa 2012/2013.
Pingamizi lingine la Yanga kwa Simba ni
kuwa imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa kwa
maelezo inao wanane wakati wanaoruhusiwa ni watano. Imewataja wachezaji
hao kuwa ni Lino Masombo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa Mude, Kanu
Mbiyavanga, Pascal Ochieng, Komalmbil Keita na Daniel Akuffor.
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za
Wachezaji ya TFF chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa inatarajia
kukutana Jumapili (Septemba 2 mwaka huu) kupitia pingamizi hizo pamoja
na usajili wa wachezaji kwa ujumla kwa 2012/2013.
LIGI KUU TANZANIA BARA 2012/2013
Michuano ya Ligi Kuu kuwania ubingwa wa
Tanzania Bara kwa msimu wa 2012/2013 itaanza Septemba 15 mwaka huu kwa
timu zote 14 kujitupa kwenye viwanja tofauti.
Mechi za ufunguzi zitakuwa kati ya Simba
vs African Lyon (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Polisi Morogoro vs
Mtibwa Sugar (Jamhuri, Morogoro), Tanzania Prisons vs Yanga (Sokoine,
Mbeya), Mgambo JKT vs Coastal Union (Mkwakwani, Tanga), JKT Ruvu vs Ruvu
Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), Kagera Sugar vs Azam (Kaitaba,
Bukoba) na Toto Africans vs Oljoro JKT (Kirumba, Mwanza).
Mzunguko wa kwanza (first round)
utamalizika Novemba 11 mwaka huu ambapo kwenye mzunguko huo mechi ya
watani wa jadi Yanga na Simba itachezwa Oktoba 3 mwaka huu kwenye Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam.
Ligi hiyo itamalizika Mei 18 mwakani kwa
mechi kati ya Toto Africans vs Ruvu Shooting (Kirumba), Mgambo JKT vs
African Lyon (Mkwakwani), JKT Ruvu vs Mtibwa Sugar (Azam Complex),
Tanzania Prisons vs Kagera Sugar (Sokoine), Simba vs Yanga (Uwanja wa
Taifa), Oljoro JKT vs Azam (Sheikh Amri Abeid Kaluta) na Polisi Morogoro
vs Coastal Union (Jamhuri).
Endapo Simba na Azam hazitafanikiwa
kuvuka hatua mojawapo ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la
Shirikisho, ratiba hiyo itafanyiwa marekebisho.
MECHI YA UFUNGUZI WA MSIMU WA LIGI 2012/2013
Mechi ya Ngao ya Jamii (Community
Shield) kuashiria ufunguzi rasmi wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa
2012/2013 kati ya bingwa mtetezi Simba na makamu bingwa Azam itachezwa
Septemba 11 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
SERENGETI BOYS KUJIPIMA KWA ASHANTI
Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini
ya miaka 17 (Serengeti Boys) iliyokuwa kambini kujiandaa kwa mechi
dhidi ya Kenya itavunja rasmi kambi yake kesho (Jumamosi) kwa mechi ya
kirafiki dhidi ya Ashanti United.
Mechi hiyo dhidi ya Ashanti United
iliyoko daraja la kwanza itachezwa kuanzia saa 10 jioni Uwanja wa
Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kwa kiingilio cha sh. 2,000.
Serengeti Boys ilikuwa Septemba 9 mwaka
huu icheze na Kenya kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya michuano ya
Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, lakini Kenya ikajitoa ambapo sasa
itacheza na Misri katika raundi ya pili. Mechi ya kwanza itachezwa
Oktoba 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Mwishoni mwa Septemba, Serengeti Boys
itarejea tena kambini kujiandaa kuikabili Misri ambapo kabla inatarajia
kupata mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya timu itakayotangazwa
baadaye.
MCHEZAJI WA MTIBWA SUGAR NAYE APATA ITC
Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu
Uganda (FUFA) limetuma Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa ajili ya
mchezaji Ayoub Hassan Isiko aliyejiunga na Mtibwa Sugar akitokea timu ya
Bull FC ya nchini humo.
ITC hiyo ilitumwa jana (Agosti 30 mwaka
huu), hivyo kufanya wachezaji ambao ITC hazijapatikana hadi sasa kubaki
wawili tu. Dirisha la usajili wa wachezaji litafungwa rasmi Septemba 4
mwaka huu.
Wachezaji ambao ITC zao bado
hazijapatikana ni Salum Kinje na Pascal Ochieng kutoka AFC Leopards ya
Kenya waliojiunga na Simba. ITC hizo zinatarajiwa kupatikana wakati
wowote kwani tayari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
limeshaziomba kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF) baada ya
nyaraka zote zilizokuwa zikitakiwa kupatikana.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Comments
Post a Comment